Makala: Yanayojiri CHADEMA Ndo Hali Halisi Au Kuna Kitu Kingine

Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema kiko kwenye matatizo. Matatizo yanayotishia uhai wake na uwepo wake kama chama cha siasa nchini. 

Kuna uwezekano mkubwa kwamba hadi hivi sasa siyo viongozi wala wanachama wa chama hicho ambao wametumia muda wa kutosha kuweza kuangalia ni tatizo gani linawakabili.

Tatizo hili ukiwasikiliza wana Chadema na hasa viongozi wao linahusishwa moja kwa moja na utendaji, sera na mwelekeo wa Rais John Magufuli kisiasa nchini. Wapinzani wanamlaumu  Rais Magufuli  kwa kudumaza upinzani  na kutaka  kuua kabisa upinzani nchini.

Kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa kwa vyama vya upinzani, na kuzuiwa kwa wanasiasa kufanya siasa nje za majimbo yao kunatajwa kama  ushahidi wa sababu zinatolewa na wapinzani.

Zaidi pia tuhuma za wanasiasa wa upinzani hasa kwenye maeneo ambayo upinzani umejijenga 'kununuliwa' na hatimaye kuachia nafasi zao za kuchaguliwa kunatajwa kama mkakati wa wazi wa Chama cha Mapinduzi-CCM, kuiua Chadema.

Miezi kadhaa sasa viongozi mbalimbali wa Chadema hasa madiwani wamekuwa wakiachia nafasi zao ambazo walizigombea miaka miwili tu nyuma na kukimbilia CCM wakidai kuwa wanaunga mkono Serikali ya Rais Magufuli.

Matukio mengine ambayo yametishia upinzani na ambayo wapinzani hasa Chadema wanayatumia kuonyesha lengo, nia na dhamira ya Serikali kuumaliza upinzani ni pamoja na mauaji ya nyota iliyokuwa imeanza kung’ara ya kiongozi wa chama hicho kanda ya magharibi aliyekuwa anaibuka kwa umaarufu Alphonce Mawazo. Tukio la mauaji ya Mawazo lilihusishwa na siasa ambalo upinzani umeendelea kudai kuwa uchunguzi wa kina haujafanyika.

Hata hivyo, tukio kubwa zaidi ambalo limewafanya wapinzani waone kuwa wamelengwa  ni jaribio la mauaji dhidi ya Mbunge Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni Tundu Lissu ambaye alishambuliwa na wale walioitwa “watu wasiojulikana” ndani ya makazi ya wabunge mjini Dodoma mchana wa jua kali.

Swali kubwa ambalo linapaswa kuulizwa; je kununuliwa kwa madiwani na wabunge peke yake kunatosha kuelezea kinachoendelea Chadema? 

Je, kuna uwezekano kuna jambo jingine ambalo linaendelea ndani ya chama hicho ambalo viongozi wake ama kwa hofu ya kufungua sanduku la pandora wanaogopa kuona kilichomo kwani hawataweza tena kulifunga? 

Je, inawezekana kuna vitu vingine ambavyo wanachama wa kawaida hawajaambiwa na kinasumbua ndani ya Chadema?

Tukio la aliyekuwa mgombea wa Chadema kwenye Urais na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kwenda kukutana na Rais hivi juzi kimewaumiza wanachama wengi na baadhi ya viongozi walikutwa hawakujiandaa na taarifa hizo.

 Baadhi ya wanachama na hata viongozi wameanza mara moja kutaka Lowassa aondolewe au aondoke huku wengi wakionekana sasa hivi hawamtaki tena. 

Kwa baadhi yetu hii inashangaza kwani miaka miwili tu nyuma viongozi na wanachama wale wale ambao walikubali kubadili gia angani walizungusha mikono na kuimba “mabadiliko-Lowassa, Lowassa – Mabadiliko”. Kwa Lowassa kwenda kukutana na Magufuli amekuwa tena si nuru, kimbilio, tumaini na nyota ya mabadiliko?

Tayari tumemsikia Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akianza kumtaja hadharani Tundu Lissu aliyeko kwenye matibabu Ubelgiji kama mtu ambaye anapaswa kubeba bendera ya Urais mwaka 2020. 

Hii itakuwa kinyume kwani tayari Chadema walishaanza kumtaja Lowassa kama mgombea wao tena? Je, watambadilishia gia Lowassa na kumchukua Lissu ambaye anaonekana kama anaweza kweli kupambana na umaarufu wa Rais Magufuli? 

Na swali jingine ambalo wapo wanaoweza kuliuliza ni je; Lissu atakuwa na tofauti ya kiutawala kumlinganisha na Rais Magufuli? Watatofautiana nini hasa? wengine wanaweza kuhoji.

Licha ya hilo, Lissu pia anatajwa kama mtu sahihi wa kurithi mikoba ya Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe ambaye ndani ya uongozi wake Chadema inajikuta mara nyingi kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa. 

Swali linaloweza kuwagawa tena Chadema ni je, wale wanaomuunga mkono Mbowe watakuwa tayari kuhamisha utii wao kwenda kwa Lissu? 

Je, inawezekana tena ukatokea mgogoro kama ule uliotokea wakati aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alipotaka kugombea nafasi ya uenyekiti ndani ya chama na kukutana ugumu ambao uliacha doa kubwa ambalo hatimaye lilimlazimisha kujiondoa na chama hicho na kwenda kuanzisha ACT-Wazalendo.

Zitto sasa ni mbunge wa Kigoma Mjini na yeye kama ilivyo Chadema anakabiliwa na kukimbiwa na viongozi wa chama chake ambao wamechukuliwa na Serikali akiwemo aliyekuwa mgombea wake wa Urais Anna Mghwira, ambaye amepewa Ukuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. 

Alifuatiwa na mmoja wa waanzilishi wa ACT ambaye walitoka na Zitto Chadema Dk. Kitila Mkumbo ambaye aliitwa na serikali na kupewa nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. 

Kijana mwingine wa chama hicho ni Mwanasheria anayepanda kila kukicha Albert Msando. Mara baada ya kujiunga na CCM Msando aliingizwa kwenye kamati ya Mwenyekiti Magufuli ambayo ameiunda ndani ya chama kwenda kufuatilia mali za CCM nchi nzima.

Ni wazi kuwa pamoja na zile zinazoonekana juhudi na mkakati wa dhati wa Serikali kudhoofisha upinzani – kitu ambacho si kigeni mahali popote duniani , Inawezekana kuna mambo mengine ambayo hayajafunguliwa vizuri na ambayo yanachangia viongozi wa upinzani walioonekana ni wapinzani kweli kujiondoa kwenye vyama vya upinzani. 

Ni mambo gani haya? Je, viongozi wa upinzani wanaweza kukaa chini na kuangalia wao wenyewe wanaongozaje, na wanafanya nini ndani ya vyama vyao kufanya wazidi kuaminiwa na wanachama na viongozi wenzao?

Je, upinzani ambao haujawa na uthubutu wa wazi wa kujitokeza kuendesha upinzani wa kweli bado unasubiria huruma na hisani ya serikali kufanya upinzani bado utaweza kuhimili mitikisiko ya miaka mitatu ijayo? 

Je, viongozi wa Chadema watakaobakia wataweza kweli kusimama na kufanya upinzani? 

Je, hawana mbinu nyingine au wamekubali masharti ya wao kufanya siasa nje ya yale yaliyowekwa na sheria na Katiba?

Au yawezekana viongozi wetu wa upinzani walichimba shimo ambalo sasa wao wenyewe hawawezi kutoka; shimo la kuvunja uaminifu na sasa wanapata shida ya kuaminiwa tena? Au kuna jingine?


from MPEKUZI

Comments