Kubenea alivyoachiwa Mahakamani Leo na kukamatwa tena na Polisi

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea leo Ijumaa aliachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kisha Jeshi la Polisi mkoani humo likamkamata tena na kumfungulia kosa lile lile alilokuwa akikabiliwa nalo.

Kubenea anatuhumiwa kuwa Julai 4 mwaka jana kumshambulia Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Juliana Shonza katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma na Julai 5, mwaka jana alifikishwa mahakamani.

Mara baada ya kufikishwa mahakamani alituhumiwa kutenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha Sheria 240 cha Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kubenea alikumbana na mkasa huo wa kuachiwa na kukamatwa leo Ijumaa mara baada ya mahakama hiyo kumwachia huru lakini baada ya kutoka nje polisi walimkamata tena na kumfungulia mashtaka yala yale ya kushambulia mbunge mwenzie Shonza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema “ni kweli tumemkamata baada ya kuachiwa huru na Mahakama na kumfungulia makosa yaleyale ya kumshambulia mbunge mwezie Juliana Shonza.”

Akizungumzia tukio hilo, Kubenea amesema “nilipoachiwa nilikamatwa na polisi kisha walinipeleka kituo cha polisi kisha wakanirudisha tena mahakamani na kufunguliwa kosa lile lile,”

“Hata hivyo nilipata dhamana kwa kudhaminiwa na mtu mmoja ambaye alisaini bondi ya Sh500,000 na mimi nikasaini bondi ya Sh500,000 na kutakiwa kurejea tena Februari 7 kesi itakaposikilizwa.”


from MPEKUZI

Comments