Jeshi la Polisi Tanzania na Msumbiji watiliana saini ya makubaliano Kuzuia Uharibifu

Jeshi la Polisi nchini limetiliana saini mkataba wa makubaliano na Jeshi la Polisi la Msumbiji kushirikiana kupambana na uhalifu katika nchi hizo mbili, hasa maeneo ya mpakani.

Mkataba huo utahusisha kubadilishana taarifa, mbinu na uzoefu katika kupambana na ugaidi na dawa za kulevya ambazo zinaathiri nguvu kazi kwenye mataifa yao.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Januari 15, 2015 kabla ya kusaini makubaliano hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP,  Simon  Sirro amesema wahalifu waliodhibitiwa katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji sasa wamekimbilia Msumbiji.

Hata hivyo, amewaonya wahalifu hao kwamba hata huko hawatakuwa salama kwa sababu Jeshi la Polisi Tanzania linashirikiana na Msumbuji katika kupambana na uhalifu kwa kubadilishana taarifa.

"Wale wahalifu waliokimbilia Msumbiji au Congo hawako salama. Majeshi yetu ya polisi yanashirikiana, ndiyo maana leo tunatiliana saini makubaliano ya ushirikiano," ameaema Sirro.

Amewataka wahalifu hao waliokimbilia Msumbiji kuachana na uhalifu kwa sababu wakiendelea watakamatwa kwa ushirikiano wa majeshi hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Msumbiji, Bernardino Rafael amesema nchi yake inakabiliwa na wahalifu kutoka nchi nyingine, hivyo makubaliano hayo yatasaidia kupunguza uhalifu.

Amesema wanataka kudhibiti mipaka yao dhidi ya wahalifu hao ambao wanahatarisha amani katika nchi hiyo pamoja na nchi za jirani.

"Watu wenye ualbino wanauawa kwa imani za kishirikina na taarifa zinaonyesha wahalifu hao wanatoka mataifa mbalimbali. Tutashirikiana na Polisi  Tanzania katika kubadilishana taarifa ili kukomesha mauaji hayo," amesema Rafael.


from MPEKUZI

Comments