Waziri Mkuu Akagua Ujenzi Wa Hoteli Pemba.....Asema Lengo Ni Kuimarisha Shughuli Za Utalii, Kuongeza Ajira

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ukarabati wa Hoteli ya Mkoani ambapo amesema lengo la maboresho hayo ni kuimarisha shughuli za utalii na kupunguza tatizo la ajira.

Amesema ili kuhakikisha lengo la Serikali linafikiwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Khamis Mussa Omar ahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

Ameyasema hayo jana  (Jumapili, Januari 19, 2020) baada ya kukagua mradi huo uliopo katika wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba. Mradi huo wenye thamani ya sh. bilioni nne unatekeleza na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF)

Waziri Mkuu amesema mradi wa ukarabati wa hoteli ya Mkoani  ni muhimu katika kuimarisha sekta ya utalii na huduma za malazi hususani kwa wageni wanaotembelea kisiwa hicho cha Pemba sambamba na kutengeneza ajira kwa wanawake na vijana.

“Ukarabati huu unatarajia kutoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya ajira, teknolojia, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha ustawi wa wananchi wetu. Endeleeni kuiamini Serikali yenu.”

Akisoma taarifa ya ukarabati wa mradi huo, Meneja Uwekezaji wa ZSSF, Bw. Abdulaziz Ibrahim Idd amesema ukarabati huo ulianza Julai 2019 na unatarajiwa kukamilika Machi 2020.

Amesema ukarabati wa jengo hilo ambalo awali lilikuwa la ghorofa moja umehusisha pia kuongeza ghorofa mbili na kufikia tatu, hali ambayo italifanya jengo hilo kuwa na vyumba 16 vya kulala kutoka vinane vya awali vikiwemo viwili kwa ajili ya watu mashuhuri.

Meneja huyo amesema kuwa mbali na kuongezeka kwa vyumba pia umejengwa ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 100, mgahawa wa kisasa pamoja na sehemu ya kufulia nguo kwa ajili ya wageni na watu wote watakaohitaji huduma hiyo.

“Kwa sasa ujenzi huu umefikia asilimia 80  na unatarajia kukamilika mwezi Machi mwaka huu. Mradi huu utakapokamilika utakuwa ni moja ya chanzo cha ajira za kudumu 50, hivyo kuinua uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.”

Hoteli hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilifunguliwa Septemba 1974 na iliendeshwa na Serikali yenyewe kwa lengo la kutoa huduma kwa wageni na hata wenyeji waliofika Pemba.

Lakini kutokana na uchakavu wake Serikali ikaamua kusitisha huduma zake na kuifunga ili kutafuta mwekezaji ambaye ataiendelea. Hoteli hiyo imekuwa haitumiki kwa kipindi cha takribani miaka 12.

Hata hivyo, Baraza la Mapinduzi chini ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein likaamua kuikabidhi ZSSF hoteli hiyo kwa lengo la kuifufua na kuiendeleza.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments