Waziri Kairuki: “Kila Mtanzania Anaweza Kuwekeza, Tumieni Fursa Zilizopo”

MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki amewaasa wananchi kuthubutu uwekezaji katika maeneo yenye tija kwa kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo ili kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao na nchi kwa ujumla.

Ametoa kauli hiyo tarehe 23 Januari, 2020 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kiwanda cha kuchakata maziwa ya mtindi cha Mather Dairies kilichopo Kijiji cha Ikwiriri Wilaya ya Rufiji katika Mkoa wa Pwani alipotembelea kiwandani hapo ikiwa ni eneo la mwisho kutembelea katika ziara yake ya siku 6 Mkoa wa Pwani.

Akiwa katika kiwanda hicho kilichowekeza mtaji wa zaidi ya milioni 300 chenye uwezo wa kuchakata zaidi ya lita 2000 kwa siku ambazo hutengeneza maziwa ya mtindi aina ya Yogurt Full Manyonyo, waziri alitoa hamasa hiyo kwa Watanzania kuzichangamkia fursa na kuwatoa shaka kuwa hakuna Mwananchi asiyeweza kuwekeza kikubwa ni kuwa na nia na uthubutu.

“Ni ukweli kuwa, kila uwekezaji Mtanzania anaweza kuufanya muhimu kuwa na ujuzi, teknolojia pamoja na mtaji pasipo kutia shaka na kujiamini,”alifafanua Waziri Kairuki

Aliongezea kuwa, ikiwa uwezo wa kuwekeza ni mdogo kwa kuzingatia ukosefu wa ujuzi wananchi wanapaswa kutumia fursa za mafunzo ya ukuzaji ujuzi unaotolewa katika vyuo mbalimbali na kutumia watu wenye uzoefu inapofaa kulingana na aina ya uwekezaji unaotaka kuufanya.

Aliwaasa watanzania kuacha tabia ya kukatishana tamaa na kuona namna ya kushikamana kuweza kuwekeza katika sekta mbalimbali.

“Kumekuwa na tabia ya kukatishana tamaa pindi mtu anapothubutu kuona fursa na kuichangamkia, ni rai yangu kwa wananchi kuona watanzania tunawekeza kufanya mambo makubwa katika maeneo yote yenye fursa, na kuzitumia vyema mamlaka zilizopo kwa kupata msaada ya ushauri elekezi na miongozo ya namna bora ya kuwekeza,”alifafanua

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Mzee Abdallah Nyarando alieleza namna alivyoanza uwekezaji wake mwaka 2010 kwa mtaji wa shilingi milioni 20 na hadi kukamilika kwa kiwanda hicho ametumia jumla ya shilingi Milioni 300, na kuweza lengo ni kuongeza thamani ya maziwa, kuzalisha ajira na kujipatia kipato.

 “Kiwanda hiki kimeweza kusaidia zaidi ya vijana 12 ambao wamekuwa wa msaada katika kuzalisha na kuuza maziwa maeneo mablimbali nchini ikiwemo; Masasi, Kibiti, Rufiji, Mtwara na Dar es Salaam,”alisema Mzee Nyarando.

Alitoa wito kwa wananchi kuondokana na hofu za kuwekeza katika maeneo mbalimbali na kueleza zipo faidi za kuwekeza katika nchi yao na kujipatia kipato ili kujikwamua kiuchumi.

Akiwasilisha taarifa yake kwa Waziri Kairuki Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Juma Njwayo alieleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kusaidia kundi kubwa la vijana katika kujikwamua kiuchumi kwa kuangalia maeneo muhimu ya uwekezaji katika Nyanja mbalimbali.

Aliongezea kuwa, wananchi hawana budi kujiajiri kwa kutumia nguvu kazi walizonazo na kuzichangamkia fursa za Wilaya yake ambazo alizibaini ni pamoja na shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara na kuwataka kuzitumia kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu muhimu ya kuvutia uwekezaji.

“Wilaya yetu ina vivutio vingi ikiwemo ardhi inayokubali mazao mbalimbali kama mahindi, mpunga, korosho, mazao jamii ya mikunde na mbogamboga  na matunda aina ya matikiti hivyo zitumieni kwa tija na kuhakikisha tunaondokana na ukosefu wa ajira,”alieleza Juma

Alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wawekezaji kuona maeneo yenye rutuba na kuwekeza katika mazao hayo na kubainisha fursa zilizopo katika ufugaji kwa kuzingatia uwepo wa mabwawa ya asili maji katika wilaya hiyo.


from MPEKUZI

Comments