Serikali Kuipatia Bilioni Mbili Kcmc Kwa Ajili Ya Jengo La Mionzi

Na. Catherine Sungura-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kuipatia kiasi cha shilingi bilioni mbili hospitali ya rufaa ya kanda KCMC ili kuweza kutoa huduma za tiba za mionzi hospitalini hapo.
 
Hayo yamesemwa jana  na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akijibu maswali kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii jijini hapo.
 
“Tumekubaliana na Katibu Mkuu kuitafuta hiyo bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mionzi (bunker) kwa hospitali hii tutawapatia”.
 
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa wizara yake inayo muelekeo kwa hospitali zote za rufaa za kanda kutoa huduma za mionzi hivyo hakutakuwa na haja ya wagonjwa wa kanda ya kaskazini kusafiri hadi Ocean road kupata huduma za mionzi.
 
“Wizara tumeanza kutoa huduma za mionzi,mwaka jana tulizindua hospitali ya Bugando,lengo letu ni kuweka huduma hizi kwenye hospitali zote za rufaa za kanda kama Mbeya  na tunafikiria kuweka na hapa kwenye hosputali ya Benjamin Mkapa”.Alisisitiza Waziri Ummy
 
Hata hivyo Waziri Ummy  amesema wizara imeweza kuwapatia hospitali ya KCMC fedha kwa ajili ya watumishi pamoja na dawa kiasi cha shilingi bilioni 5 katika kipindi cha miezi sita.”Kama serikali itaendelea kuthamini suala la ubia katika utoaji wa huduma za afya na mashirika ya dini na watu binafsi”.
 
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC Dkt. Gilliard Masenga amesema kuwa asilimia sitini ya wagonjwa wa saratani wanahitaji huduma ya mionzi na hospitali  hiyo imeweza kuona jumla ya wagonjwa 4323 kwa kipindi cha mwaka jana na kufanya uchunguzi wa magonjwa ya saratani ambapo kati yao watoto 239 na watu wazima ni 4084,aidha wamefanya kampeni maalum ya upimaji na ushauri katika wilaya ya Arumeru na watu 307 walipatiwa huduma ya uchunguzi wa awali wa saratani


from MPEKUZI

Comments