Rais Xi asema virusi vya corona ni changamoto kubwa....56 Wafariki Dunia

Rais wa China Xi Jinping amesema nchi yake inakabiliwa na "hali mbaya," wakati ambapo virusi vya corona vinaendelea kuenea huku watu wapatao 1,975 wakiliripotiwa kuwa wameambukizwa.

China mnamo siku ya Jumapili ilizidisha vizuizi vya usafiri ili iweze kupambana na virusi vya corona ambavyo Rais Xi Jinping amesema ni tishio kubwa. Kwa mujibu wa shirika la habari la taifa, serikali ya China imesimamisha shughuli  za kuwatembeza watalii kutoka mataifa ya nje, pia hakutakuwepo na safari za mabasi yanayotoka na kwenda mikoani kuanzia Jumapili katika juhudi za kupunguza kuenea kwa ugonjwa unaosabbabishwa na virusi vya corona.

Mlipuko huo unaaminika kuwa ulianzia katika eneo la mashariki mwa China katika mji wa Wuhan na umesambaa hadi katika nchi zingine kadhaa kama Marekani, Ufaransa, Japan na Australia.

Watu wapatao 1,975 wanaaminika kuwa wameambukizwa, na takriban vifo 56 vimeripotiwa. Taarifa ya serikali  imesema watu 324 wamo katika hali mbaya. Wakati huo huo serikali ya China imechukua hatua ya kuweka marufuku ya kuingia au kutoka kwenye mkoa wa Hubei ulio katikati mwa nchi hiyo ambao pia umeathiriwa vibaya, hii ikiwa ni katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi.
 
Kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam, ametangaza hali ya dharura kuhusu virusi vya corona katika jiji hilo na serikali yake imetangaza kufungwa shughuli za usafiri, shule na vyuo vikuu. Visa vitano vya maambukizi ya virusi vya corona vimeripotiwa katika jiji la  Hong Kong na watu zaidi ya 122 wanadhaniwa kuwa na virusi hivyo.

-DW


from MPEKUZI

Comments