Naibu Waziri Ulega Asisitiza Utengenezaji Zaidi Wa Bidhaa Za Ngozi Hapa Nchini

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara yake itahakikisha matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ya nchi kuuza ngozi na bidhaa zake kwenda nchi za nje yanafikiwa.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati alipotembelea Kiwanda cha kuchakata ngozi cha Ace Leather kilichopo katika Manispaa ya Morogoro na kujionea maboresho makubwa ya kiwanda hicho kwa kufungwa mashine za kisasa, Mhe. Ulega amesema wizara itahakikisha pia uwezekano wa kupunguza gharama kununua bidhaa za ngozi kutoka nchi za nje kuja hapa nchini zinapunguzwa.

“Matamanio ya serikali ya Rais Magufuli kila mara amekuwa akizungumzia kuhusu zao la ngozi, nchi yetu ina mifugo mingi sana na kila mara matamanio yake kuona Tanzania haitumii tena gharama kubwa kununua bidhaa za ngozi kutoka katika mataifa ya nje bali sisi ndiyo tuwauzie ngozi na bidhaa zake.” Amesema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amesema ameridhishwa na mitambo ya kisasa inayofungwa katika Kiwanda cha Ace Leather ambacho kinatarajiwa kufunguliwa tena hivi karibuni baada ya kusitisha shughuli zake ili kupisha maboresho ya kiwanda hicho kwa kufungwa mitambo hiyo ya kisasa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa makampuni ya Taifa Group of Companies inayomiliki kiwanda hicho Bw. Abdulkarim Shah amesema mara baada ya kiwanda hicho kukamilika maboresho yake kitakuwa ni moja ya viwanda vikubwa katika ukanda wa kusini mwa janga la sahara.

Bw. Shah amesema mara baada ya kiwanda hicho kukamilika kinatarajiwa kuajiri takriban wafanyakazi 250 hadi 300 na nia ya kiwanda hicho katika siku zijazo ni kuanza kutengeneza bidhaa za ngozi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amekagua pia ujenzi wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Nguru Hills kilichopo katika Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro ambapo amesema ameridhishwa na ujenzi wa kiwanda hicho.

Kufuatia ujenzi wa viwanda vya kuchakata nyama vinavyojengwa maeneo mbalimbali hapa nchini, Naibu Waziri Ulega amehamasisha wananchi kufanya biashara ya kunenepesha mifugo kwa kuwa viwanda hivyo mara vitakapokamilika vitahitaji mifugo mingi kwa ajili ya uchakataji.


from MPEKUZI

Comments