Naibu Waziri Mabula Azindua Mpango Kabambe Wa Mji Wa Tunduma

Na Munir Shemweta, WANMM TUNDUMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezindua Mpango Kabambe wa miaka ishirini (2015-2035) wa Mji wa Tunduma katika mkoa wa Songwe na kuzitaka halmashaur zote nchini ambazo hazijaadaa mipango kabambe katika Miji yao kuandaa mpango kabambe ili kuongeza kasi ya kupanga na kupima miji yote Tanzania .

Naibu Waziri Mabula amezindua Mpango huo Kabambe wa Mji wa Tunduma jana katika mji wa Tunduma wilaya ya Momba mkoa wa Songwe wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Alisema, kukamilika kwa mpango kabambe wa mji wa Tunduma kumekuja wakati muafaka kwa kuwa mpango huo utachochea utumiaji fursa na rasilimali zilizopo Tunduma na kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi sambamba na kupunguza au kumaliza migogoro ya ardhi.

‘’Mpango huu utachochea utekelezaji wa malengo ya muda mrefu ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati wa viwanda na hii inajidhihirisha katika mpango kabambe wa Mji wa Tunduma pale jumla ya hekta 4190 sawa na asilimia kumi ya maeneo yaliyopangwa kwa matumizi ya ardhi zimetengwa kwa ajili ya viwanda’’ alisema Waziri Mabula.

Alitoa wito kwa Halmashauri na wadau wa maendeleo katika mji wa Tunduma kuandaa mkakati wa mpango kazi wa utekelezaji Mpango Kabambe sambamba na kutafuta wabia na wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zilizoainishwa katika Mpango huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemus Mwangela alisema Mapango Kabambe wa Mji wa Tunduma ni muhimu kwa mji huo kwa kuwa uko mpakani na una shughuli nyingi huku asilimia sabini ya mizigo ikipitia katika mji huo.

Alisema, Mji wa Tunduma unahitaji kutazamwa kwa macho mawili kwa kuwa muingiliano wa wananchi wa Tanzania na nchi za SADC ni mwingi na kusisitiza katika mkoa wake Mji wa Tunduma ni wa kwanza kuandaa Mpango Kabambe. 

Akielezea Mpango huo Kabambe wa Mji wa Tunduma, Katibu Tawala wa wilaya ya Momba Mery Marcko alisema, lengo la mpango huo ni kuwa kitovu cha biashara kwenye mkoa wa Songwe, Nyanda za Juu Kusini na Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na kutaja maeneo ya kimkakati kuwa ni Kati Kati ya Mji wa Tunduma, Miji ndani ya Mji yaani Satellite Towns, Ukanda Maalum wa Kibiashara na Ukanda wa Viwanda.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala wa Wilaya ya Momba, jumla ya miradi 24 itatekelezwa katika awamu ya kwanza (2015-2020) na kuitaja baadhi yake kuwa ni Kituo cha Mabasi cha Mpemba ambacho ujenzi wake umeanza, Barabara ya lami kutoka Mpemba hadi Isongole itakayounganisha eneo la Mpemba na nchi jirani ya Malawi kupitia Isongole (Ileje), Ujenzi wa hospitali ya Mji wa Tunduma na ukamilishaji ujenzi wa miundo mbinu ya maji  pamoja na ujenzi wa maegesho ya malori unaojengwa katika kata ya Chapwa. 


from MPEKUZI

Comments