Waratibu Elimu Wazembe Kuchukuliwa Hatua Kali Mkoani Songwe

Waratibu Elimu kata na Wasimamizi wa Sekta ya Elimu Mkoa wa Songwe waliobainishwa katika ripoti ya uchunguzi wa hali ya sekta ya Elimu kuwa ni wazembe katika kusimamia maendeleo ya elimu watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila amesema hayo jana wakati wa kikao na Waratibu Elimu Kata na Maafisa Elimu ili kutathmini maendeleo ya Sekta ya Elimu kwa mwaka 2019 na kupanga mikakati ya kuboresha elimu kwa mwaka 2020.

“Tuliwapa kazi wadhibiti ubora ya kufanya uchunguzi kwanini Mkoa wetu haufanyi vizuri kielimu na ripoti yao imebainisha uwepo wa uzembe wa waratibu elimu Kata katika usimamizi, sasa nitachukua hatua kali kwa waratibu elimu wote wazembe.”, amesema Kafulila.

Kafulila amesema Waratibu Elimu kata wote walisaini Mkataba ambao uliwataka kusimamia Sekta ya elimu na kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda lakini pia serikali imewawezesha posho na usafiri lakini wapo baadhi yao ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao.

“Serikali imewapa posho na Waratibu Elimu Kata lakini baadhi yao wamebainishwa katika ripoti kuwa wanafanya kazi kwa kuogopana na kuendekeza urafiki, hawawachukulii hatua walimu na wakuu wa shule ambao hawatimizi majukumu yao, hao hatuwezi kuwavumilia.”, amesisitiza Kafulila.

Naye Mwenyekiti wa Wadhibiti Ubora wa Elimu Mkoa wa Songwe Mwalimu Jackson Lwafu amesema walitathmini kwanini baadhi ya shule katika Mkoa wa Songwe zimeshuka kielimu na walibaini kuwa usimamizi dhaifu umechangia kwa kiasi kikubwa.

Lwafu amesema endapo wasimamizi wa Elimu Mkoa wa Songwe watatambua majukumu yao na kuyasimamia, maendeleo ya sekta ya Elimu Mkoa wa Songwe yatakuwa mazuri.

Mratibu Elimu Kata ya Mkukwe Wilayani Songwe Mwalimu Judith Mwasoke amesema taarifa ya wathibiti ubora inasikitisha kwakuwa ili kuwe na mafanikio lazima taratibu zifuatwe hivyo suala la kuoneana aibu na kuogopana halifai na waratibu Elimu Kata wenye tabia hiyo waache.

Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma Mtafya Wilson amesema kwa mwaka 2020 watahakikisha walimu wanafundisha vipindi vyote pamoja na kuwasimamia Waratibu Elimu Kata wanatimiza wajibu wao.

Afisa Elimu Mkoa wa Songwe Juma Japhet Kaponda amesema Matokeo ya darasa la saba mwaka 2019 hali haikuwa nzuri kwakuwa Mkoa ulipanda ufaulu kwa asilimia 1.65 kwa kuwa na ufaulu wa asilimia 75 na Mkoa ukishika nafasi ya 21 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2018 wa asilimia 73 na nafasi ya Mkoa wa Songwe ilikuwa 17.


from MPEKUZI

Comments