Sikonge Wapigwa Marufuku Kulima Pamba Hadi Serikali Itakapotoa Tamko La Kuwaruhusu

NA TIGANYA VINCENT
WAKULIMA wilayani Sikonge ambao wanataka kulima zao la pamba wametakiwa kuwa wavumilivu hadi hapo utafiti utakapokamika ili Serikali ijiridhishe kama tishio la mdudu aina ya funza mwekundu halipo katika maeneo jirani yaliyopigwa marufuku kulima zao hilo.

Ushauri huo umetolewa juzi wilayani Sikonge na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa kikao robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani.

Alisema kwamba Wizara iliweka karantini kwa Wilaya zinazopakana na mikoa ya Rukwa na Mbeya kutolima pamba kutokana na kuwepo funza wekundu wanaoshambulia zao hilo.

Mkuu wa Mkoa alisema hawezi kuruhusu watu walime hadi hapo wataalamu wa Wizara waje wajiridhishe na watoe tamko kuhusiana kutokuwepo kwa tishio la mdudu huyo.

Katika agizo lake Mkuu wa Mkoa aliwataka Madiwani wasiende kuwahamasisha wananchi kulima zao la pamba kabla hawajapata msimamo wa Serikali ili wasijekupata hasara.

Mwanri alisema kitendo cha kuruhusu kulimwa kwa zao hilo kabla ya matokeo ya wataalamu hayajatoka  kunaweza kusababisha hasara kubwa katika maeneo ya ndani na nje ya Mkoa wa Tabora ambapo funza huyo mwekundu anaweza kusabambaa hata katika maeneo ambayo alikuwa hayupo.

Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Peter Nzalalila aliishauri Serikali iwaruhusu walime  pamba kama zao mbadala ya tumbaku ambayo inapigwa vita kimataifa.

Aliomba Serikali iwaruhusu kulima pamba kwa kuwa maeneo ya jirani zao ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku wameanza kulima na wana vyama vya Msingi vya zao hilo.

Nzalalila alisema wakazi wengi wamehamasika kulima pamba wanachosubiri kibali ili waweze kushiriki kilimo hicho kwa ajili ya kuondokana na umaskini.

Katika hatua nyingine Madiwani na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge wametakiwa kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kuwahimiza wananchi kujielekeza katika kulima kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuzalisha chakula na mazao ya biashara ya kutosha ambayo yatawasaidia kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao.

Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa kipindi hiki ndio maana amesimamisha kwa muda likizo za Maafisa Ugani na Kilimo ili waweze kutoa ushauri utakaomsaidia mkulima kulima kisasa.

Mwisho


from MPEKUZI

Comments