Mazingira Ya Uwekezaji Katika Sekta Ya Mifugo Na Uvuvi Yaboreshwa Zaidi

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema serikali ya awamu ya tano imefanya kazi kubwa ya kuandaa mazingira ya biashara za ndani ziweze kufanya vizuri zaidi.

Akizungumza jana (06.12.2019) wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya serikali, wawekezaji na wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Ulega amesema serikali imeweza kudhibiti matumizi ya fedha kununua nyama, maziwa na samaki kutoka nje ya nchi ili kutosheleza soko la ndani.

Akifafanua katika kikao hicho ambacho kimeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki ambaye amekuwa mwenyekiti katika mikutano ya namna hiyo iliyofanyika pia katika mikoa ya Morogoro na Pwani, Mhe. Ulega amesema serikali imekuwa ikitumia takriban Shilingi Bilioni 10 kuagiza nyama kutoka nje ya nchi, Shilingi zaidi ya Bilioni 100 kuagiza samaki na zaidi ya Shilingi Bilioni 50 kuagiza maziwa, kitendo ambacho kwa sasa serikali haitumii fedha hizo tena kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Katika mkutano huo ambao umehusisha mawaziri na naibu mawaziri kutoka zaidi ya wizara 10, Mhe. Ulega amesema serikali imeendelea kuweka mazingira shindani ili kutoa fursa ya uwekezaji katika sekta ya ufugaji na uvuvi, hatua ambayo katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano Benki ya Kilimo (TADB) imeweza kupata maombi ya mikopo ya zaidi ya Shilingi Bilioni 90 na kufanikiwa kusajili na kutoa mikopo ya Shilingi Bilioni 25.3 ambapo Shilingi Bilioni 23 kwa ajili ya sekta ya mifugo na takriban Shilingi Bilioni Mbili kwa sekta ya uvuvi ambayo miaka iliyopita haikuwahi kukopeshwa kiasi chochote cha fedha ilhali sekta ya mifugo iliwahi kukopeshwa kiasi kisichozidi Shilingi Bilioni Tisa pekee.

Naibu Waziri huyo ametoa fursa kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaotaka kuwekeza katika sekta ya uvuvi kupitia ufugaji wa samaki, ambapo hitaji la samaki kwa mwaka ni Tani 800,000 wakati Tanzania inaweza kuzalisha wastani wa Tani 400,000 hadi 450,000 aidha amewataka pia kuwekeza katika viwanda vya maziwa, nyama na ngozi.

Katika kuhakikisha wanapata miongozo sahihi ya uwekezaji Naibu Waziri Ulega amewataka wadau kutumia Dawati la Sekta Binfasi lililo chini ya wizara hiyo, ili kufahamu juu ya kanuni, miongozo na tozo wakati wa uwekezaji wao.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments