Kijana Wa Kazi Amuibia Bosi Wake Hati Na Kuikopea

Na. Hassan Mabuye, WIZARA YA ARDHI-Iringa
Mkazi wa Iringa mjini Bi. Lugano Mwadini amejikuta katika deni linalopelekea karibu nyumba yake kupigwa mnada baada kijana wake wa kazi kukopa pesa kiasi cha shilingi 1,000,000 kwa kutumia hati yake ya umiliki wa ardhi ambayo amemuibia.

kadhia hiyo imetokea wakati wa mkutano wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kupitia programu yake ya 'Funguka kwa Waziri' mkoani Iringa alipokuwa akisikiliza na kutatua kero za ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Iringa katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo katika Manispaa ya Iringa.

katika mkutano huo Bi. Lugano alimtuhumu Kijana wake wa kazi kwa kumuibia hati na kuenda kukopa kwa Bw. Laurence Panklas ambaye ni askari wa jeshi la polisi mkoani Iringa anayekopesha kwa riba ya 400,000 kila mwezi ambazo kijana huyo hakuweza kuzirudisha kwa wakati jambo lililopelekea kutaka kuuzwa kwa nyumba yake ili kufidia deni hilo.

Bi. Lugano Mwadini aligundua hayo baada ya kupigiwa simu na mkopeshaji huyo kumtaka kwenda kubalisha umiliki wa hati hiyo ili apewe mtu mwingine kwa kuwa hati yake imekopewa na inadaiwa shilingi 1,400,000.

"Mi nilikuwa sipo lakini nikaja kupata taarifa kwa kupigiwa simu kwamba kijana wangu wa kazi ameniibia hati yangu wakati nikiwa katika kazi zangu na amekopea kwa askari mmoja ambaye anakopesha kwa riba ya laki nne kila mwezi, kwa hiyo kijana wangu anadaiwa 1,400,000 na hajalipa hadi sasa" Alisema Bi. Lugano Mwadini.

Waziri Lukuvi alimuagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Iringa Juma Bwire kushughulikia suala hilo, kwanza kwa askali wa jeshi la polisi ambaye anafanya biashara ya pesa na kama ana kibali cha biashara hiyo na analipa kodi, kama halipi basi alipe kodi kwa miamala yote aliyowahi kufanya.

Aidha Waziri Lukuvi aliagiza kukamatwa kwa kijana huyo wa kazi ili alipe deni hilo kwa Bosi wake na kueleza kwanini amefanya uhalifu huo wa kuiba hati ya mtu mwingine.

Katika mkutano huo Waziri Lukuvi aliweza kusikiliza na kutatua migogoro ya wakazi wa mkoani Iringa takribani 200 kwa siku moja ambapo baadhi ya wananchi walieleza kuridhishwa kwa juhudi za waziri lukuvi kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi ya wakazi wa maeneo mbali mbalibila nchini bila kubagua.


from MPEKUZI

Comments