Jamii yaombwa kuwashika mkono watoto yatima

Na Amiri kilagalila-Njombe
Jamii nchini inaombwa kuendelea kutoa mchango katika vituo vya kulea watoto yatima pamoja na kusaidia watoto katika malezi,ili kuendelea kupunguza changamoto zinazovikabili vituo vya kulea watoto nchini.

Ombi limetolewa na baadhi ya walezi wa vituo vya kulea watoto yatima Njombe mjini mara baada ya hafla ya chakula cha mchana baina ya vituo vya kulea watoto mjini humo pamoja na viongozi wa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii wa mji wa Njombe iliyofanyika katika kituo cha kulea watoto yatima cha St.Anne kilichopo Uwemba mjini humo.

Sista Maria Mgeni ni msimamizi wa shule ya watoto yatima mtakatifu Donbosco iliyopo Unewa kijiji cha Madobole kata ya Luponde,anasema licha ya serikali na baadhi ya wahisani kutoa michango ya hali na mali ili kuendeleza vituo hivyo lakini bado wanaiomba jamii kuendelea kujitoa kwa kuwa bado changamoto zinaendelea kukabili vituo.

“Ningeomba msaada jamii iendelea kuchangia chochote iwe mavazi,chakula,vitanda, hata Magodoro na kwa upande wa serikali hasa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kwa kweli tunawashukuru sana kwa kuendelea kuwa pamoja na sisi”Alisema Maria Mgeni

Naye Sista Maria Mwinuka kutoka kituo cha kulea watoto yatima St.Anne,amesema wameweza kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuokoa maisha ya watoto wengi wanaofika kituoni wakiwa na hali mbaya huku akiomba jamii ijifunze kuwajibika katika kuwalea watoto.

“Wito wetu jamii ijifunze kuwajibika kulea mtoto,katika familia za kiafrika watoto hulelewa na jamii kwa hiyo mama akifariki,ndugu pande zote mbili wahusike kumlea kwa karibu mtoto katika mazingira ya nyumbani”alisema Sista Maria Mwinuka

Enembora Lema ni afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya mji wa Njombe,amesema serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na vituo kwa ajili ya malezi ya watoto hivyo ametoa pongezi kwa kazi zinazofanywa na walezi.




from MPEKUZI

Comments