Faida za muungano wa Tigo na Zantel kwa watumiaji wa simu za mkononi nchini


Imetangazwa mapema wiki hii kuwa kampuni mbili kubwa za mawasiliano ya simu nchini Tanzania za Tigo na Zantel zimeungana.

Muungano huo wa kampuni hizi mbili unafanya ziunganishe huduma zao maeneo yote mawili ya Muungano kwa maana ya Bara na Visiwani na ni muungano ambao umekuwa ukisubiriwa kutokea. 

Mapema mwaka huu wakurugenzi wa kampuni hizo mbili waliweka bayana kusudio hilo la kuungana katika mahojiano na jarida maarufu duniani la Forbes toleo maalumu la kujenga Tanzania yenye mafanikio.

Waliweka wazi namna gani muungano huo utaleta faida kwa wateja wa kampuni hizo mbili kupitia kuboresha huduma kwa kiwango cha juu na sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi kwa ujumla. 

Swali ni je muungano huu una faida gani hasa kwa mteja?  

Kwa ufupi, wateja wa kampuni hizi zote mbili sasa wataweza kufurahia huduma bora zaidi ambazo zitatolewa kutokana na muungano huu. Muungano huu unaleta nguvu za kampuni zote mbili pamoja na kutoa kilicho bora zaidi kote bara na visiwani, mijini na vijijini. Pia unaongeza wigo wa kufanya biashara toka pande zote mbili. Lakini ni vyema pia kufahamu faida hizi za muunganiko si tu kwa wateja wa Tigo na Zantel pekee. 

Akielezea kuhusu muungano huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo Tanzania , Simon Karikari, amesema kuwa anaamini “utatengeza sekta bora zaidi ya mawasiliano ya simu za mkononi nchini Tanzania kwa sasa na siku za usoni.” Ameongeza pia kuwa soko lenye kampuni zilizoungana kama hivi litasukuma mbele ubunifu. 

Wataalamu wa uchumi na teknolojia wameweka bayana athari hasi za kuwa na soko vipande vipande au lenye kampuni nyingi za mawasiliano ya simu za mkononi mijawapo ikiwemo kushindwa kuwekeza mitaji mikubwa yenye kukuza tija kwa mtumiaji kwa muda mrefu. 

Muungano wa Tigo na Zantel ni hatua kubwa na muhimu katika kukuza sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi nchini Tanzania na kuleta mabadiliko chanya katika sekta hii. Sasa zimebaki kampuni tano badala ya sita kutokana na kuondoka kwa kampuni ya Smart mwezi jana. Hatua ya Tigo na Zantel sio tu muhimu kwa wateja wao bali pia uchumi wa nchi na sekta ya mawasiliano kwa ujumla.


from MPEKUZI

Comments