Dkt. Ndugulile: Ukatili Wa Kijinsia Ni Ujambazi Mpya

Na Mwandishi Wetu Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Maeandeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema Mwaka 2017 Tanzania ilikuwa na matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia takribani 41elfu na kati ya vitendo hivyo ukatili dhidi ya watoto pekee ni 13 elfu.

Naibu Waziri Ndugulile amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari wakati wa Semina ya wabunge wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Vitendo vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto Jijini Dodoma.

Aidha Naibu Waziri Ndugulile ameifananisha changamoto ya vitendo vya ukatili Nchini kuwa ni ujambazi mpya unaozidi kuwakumba wanawake na watoto kutokana na vitendo hivyo kuendelea kutokea katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.

Dkt. Ndugulile amesema unapoongelea ukatili wa kijinsia unazungumzia maeneo makubwa matatu ambayo ni ukatili wa kimwili, kisaikolojia na ukatili wa kiakili na kuongeza kuwa changamoto ya ukatili wa kijinsia imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Ameyataja matendo hayo yanayozidi kuongezeka kuwa ni mimba na ndoa za utotoni, ubakaji na ulawiti dhidi ya wanawake na watoto ndio maana ili kukabiliana na vitendo hivyo serikali tangu mwaka 2016 ilianzisha Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Vitendo vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa juhudi za Serikali katika utoaji elimu bure hapa nchini umepunguza suala la mimba na ndoa za utotoni kwa kuwa mtoto wa kike anapozidi kukaa shuleni ndivyo uwezekano wa mimba za mapema unapozidi kuwa mdogo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba amewambia wajumbe wa Kamati hiyo na Wizara kuwa jamii bado ina mila potofu zinazoendeleza vitendo vya ukatili kama vile ukeketeji na kuwataka Wabunge kuelimisha Jamii dhidi ya Vitendo hivyo.

Aidha Mhe. Serukamba amelitaja suala la elimu kwa umma kuhusu utokomezaji wa vitendo vya ukatili kupewa kipaumbelae huku akisifu mpango wa Serikali wa kutokomeza umasikini kwa kiwango cha kaya kupitia TASAF na kuongeza kuwa umasikini pia ni chanzo cha ukatili dhidi ya wawanawake na watoto.

Naye Mshauri Mbobezi wa Sera na Mipango kutoka Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa Tanzania Bi. Usu Malya amesema shirika lake litaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya Idara Kuu Maeandeleo ya Jamii kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hapa nchini.

Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto ulianza tangu mwaka 2016 na umewezesha kuwa na mtazamo wa pamoja katika utekelezaji wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuondoa mwingiliano, upotevu wa rasilimali watu, fedha na muda unaotumika katika kushgulikia suala moja.


from MPEKUZI

Comments