Chama cha ACT-Wazalendo Chalalamika Wagombea Wake Kuenguliwa Bila Sababu...Kamati Kuu Ya Chama Hicho Kukutana Leo

Chama  cha ACT-Wazalendo kimeeleza kufadhaishwa na kile kilichokiita hujuma dhidi ya vyama vya upinzani katika uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu, alidai kuenguliwa kwa wagombea wao, kulipangwa mapema ili wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wapite bila kupingwa.

“Wagombea wetu 110,040 nchi nzima wameenguliwa, wakiwamo 2,000 ambao hata sababu za kuenguliwa kwao hazijaelezwa.

"Kuenguliwa kwa wagombea hawa na wengine kutoka vyama vya upinzani kumelenga kuhakikisha wagombea wa CCM wanapita bila kupingwa," alisema Semu.

Akifafanua zaidi kuhusu kuenguliwa kwa wagombea wa chama chake, kiongozi huyo wa ACT alidai baadhi ya wagombea wao wameambiwa hawana shughuli halali licha ya kuwa miongoni mwa walipakodi wakubwa nchini.

Alidai miongoni mwa walioenguliwa kwa kigezo hicho ni mgombea wao katika Mtaa wa Masaki jijini, ambaye jina lake limekatwa licha ya kuwa ni mfanyabiashara anayetambuliwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) na hulipa kodi ya zaidi ya Sh. milioni 30 kwa mwaka.

Alidai kuna wagombea wao wameenguliwa kwa kuelezwa kuwa chama hicho hakipo katika orodha ya vyama vilivyosajiliwa kwa msajili wa vyama nchini.

Semu pia alisema kuna walioenguliwa kwa madai kuwa si wakazi wa maeneo wanayogombea licha ya kuzaliwa katika maeneo hayo na kuwa na makazi ya kudumu na familia zao kuishi katika maeneo husika.

"Kuna hujuma pia ilifanyika kwa fomu za wagombea wetu kughushiwa na kuongezwa herufi za majina ya mgombea na hivyo mgombea kuenguliwa kwa maelezo kuwa majina yaliyotumika siyo sahihi licha ya kuwa fomu hizo zilijazwa majina sahihi," alidai.

Alisema tayari chama hicho kimeanza kuchukua hatua dhidi ya suala hilo kwa kufanya mawasiliano na vyama vingine, vikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National League for Democracy (NLD) na Chama cha NCCR-Mageuzi ili kuunganisha nguvu na kuchukua hatua za pamoja.

Aliongeza kuwa kamati ya chama imeitishwa kwa dharura na itakuwa na kikao leo ili kutafakari hatua za kuchukua kukabiliana na kile alichoita hujuma dhidi ya vyama vya siasa nchini.



from MPEKUZI

Comments