Ajali Yaua Watu Watatu Arusha

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia dereva wa gari ndogo aina ya Toyota Salon yenye namba za usajili T.213, Deogratius Thomas Kiwale, aliyesababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wawili baada ya gari lake kuacha njia na kugonga wafanyabiashara na watembea kwa miguu.

Taarifa hiyo imetolewa Novemba 9, 2019 na Kamanda wa Polisi mkoani humo ACP Jonathan Shanna, ambapo amesema kuwa ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia jana  majira ya saa 1:00 usiku, katika barabara ya Arusha Moshi maeneo ya Manchester, Kata ya Sekei Halmashauri ya Jiji la Arusha.

"Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari lake hali iliyopelekea vifo na majeruhi, Dereva wa gari hilo amekamatwa na pindi upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria" amesema ACP Shanna.

ACP Shanna ameyataja majina ya watu waliofariki na kupatwa na majeraha katika ajali hiyo kuwa ni Gudla Mashanga, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari, Honorina Zakaria, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari, Amina Hassan mkazi wa Moivo, ambapo majeruhi ni Rogath Minja, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari na Renatha Thadei ambaye pia ni mfanyabiashara na mkazi wa Sekei.

Kwa mujibu wa Kamanda Shanna, miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru, na majeruhi pia wamelazwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi.


from MPEKUZI

Comments