Waziri Mkuu Aeleza Jinsi Ya Kufikia Nchi Ya Kipato Cha Kati

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ili Tanzania ifikie lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati inayoongozwa na uchumi wa viwanda, haina budi kuhakikisha kuwa inatimiza vigezo kadhaa, kikiwamo cha ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha asilimia 12 kwa mwaka.

Amesema vigezo vingine ni mchango wa viwanda katika Pato la Taifa usiopungua asilimia 15; utoaji ajira rasmi na za moja kwa moja uongezeke na kufikia asilimia 40 ya ajira zote; na sekta ya viwanda iweze kuiingizia nchi mapato ya fedha za kigeni zaidi ya asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.

Alitoa kauli hiyo jana usiku (Alhamisi Oktoba 17, 2019) wakati akizungumza na wageni na washiriki waliohudhuria hafla ya utoaji Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora wa mwaka 2018 iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli alisema: “Ili kufikia vigezo hivyo na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya viwanda, ni lazima tujizatiti na kuimarisha ushirikiano wa karibu baina ya sekta ya umma na sekta binafsi,” huku akiwasihi washiriki katika hafla hiyo waitumie fursa hiyo kutafakari mbinu mpya za kufikia vigezo hivyo muhimu vya kuijenga Tanzania mpya ya viwanda.

“Kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa sekta ya viwanda katika kukuza uchumi wa nchi yoyote duniani. Viwanda ndivyo vimekuwa chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi mbalimbali duniani na mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuondoa umasikini kwa kutoa ajira nyingi na za uhakika kwa wananchi. Maendeleo ya sayasi na teknolojia yanategemea sana sekta ya viwanda.”

“Takwimu pia, zinaonesha kwamba katika mwaka 2018, sekta ya viwanda imetoa ajira rasmi 306,180 ikilinganishwa na ajira 280,899 za mwaka 2017; sawa na ongezeko la asilimia tisa. Tutaendelea kuchukua hatua zinazostahiki ili kuwezesha sekta hii ikue kwa haraka na kutoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini wa wananchi wetu,” alisema Waziri Mkuu.

Aliema kutokana na jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali za kujenga uchumi wa viwanda, jumla ya viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa katika mikoa mbalimbali. “Viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi (saruji, nondo, vigae, mabomba, marumaru, n.k); pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ikiwemo nafaka, matunda, mafuta ya kupikia na bidhaa za ngozi,” alisema.

Alisema viwanda vingi vimeanzishwa nchini na ni faraja kuona wawekezaji wa ndani nao wanaendelea kufungua viwanda vipya pamoja kuongeza uwekezaji wao. “Moja ya viwanda vinavyohamasishwa ni vile vinavyochochea uzalishaji wa ajira kwa wingi. Ujenzi wa viwanda vipya nchini, katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano, umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 nchi nzima,” alisema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wenye viwanda na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Innocent Bashungwa alisema wizara yake kwa kushirikiana na sekta binafsi itaendelea kuondoa kero zinazokwamisha ufanisi na ukuaji wa sekta ya viwanda zikiwemo kero kubwa zinazolalamikiwa na sekta hiyo.

Alizitaja baadhi ya kero hizo kuwa ni ucheleweshaji wa malipo ya madai ya kodi za ongezeko la thamani (VAT) na asilimia 15 ya ziada inayolipwa na waagizaji wa sukari ya viwandani; ushindani usio na uwiano na bidhaa za bei nafuu kutoka nje ya nchi kama vile nondo, mabomba ya plastiki, nguo na mavazi, bidhaa za ngozi na marumaru.

“Pia tutaangalia upya uwepo wa utitiri wa tozo na ada za juu zinazotozwa na taasisi mbalimbali za Serikali, ongezeko la kodi ya kuagiza mali ghafi kutoka nje ya nchini, na kucheleweshwa upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi kwa wataalam wa kigeni wasiopatikana hapa nchini (expetriates employees),” alisema.

Kuhusu usajili wa makampuni, Waziri Bashungwa alisema Wizara hiyo kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imekamilisha kuweka mifumo ya kusajili majina ya biashara kwa njia ya mtandao. “Mifumo hiyo inawawezesha wafanyabiashara kusajili jina la biashara, uandikishwaji wa makampuni, usajili wa alama za biashara na usajili wa viwanda mahali popote walipo kupitia tovuti ya wakala (www.brela.go.tz).”

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Bw. Subhash Patel, alisema CTI inaunga mkono azma ya Rais Magufuli ya kuleta viwanda nchini. “Hakuna nchi itakuwa imefanikiwa duniani bila kuwekeza kwenye viwanda,” alisema.

Akielezea uwepo wa fursa za biashara kwa wawekezaji wa Kitanzania, Bw. Patel alisema Tanzania ina majirani ambao hawana bandari na hiyo ni fursa tosha ya kuwekeza na kuendeleza biashara kwenye nchi jirani.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI

Comments