Waziri Mhagama Azitaka Halmashuri Kuhakiki Taasisi Ndogo Za Fedha Kubaini Taasisi Zinazowaibia Wananchi

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu , Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Jenista  Mhagama , ameziagiza  halmashauri zote nchini kufanya uhikiki wa kina wa taasisi ndogo za kifedha zinazotoa mikopo  kwa wananchi na vikundi, ili kuzibaini  taasisi zinazowaibia Watanzania badala ya kuwanufaisha kiuchumi..

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo, katika kilele cha Maonesho ya tatu ya Mifuko/ Programu za Uwezeshaji na Vikundi vya Kifedha vya Kijamii, yaliyofanyika Kitaifa katika  Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Oktoba 20, 2019.

“Ninajua baadhi ya taasisi ndogo za fedha badala ya kuwasaidia  wanachama zimekuwa ziifanya kazi ya kuiba fedha za wanachama  na kuwafanya wanachama warudi nyuma badala kusonga mbele, agizo hili Baraza la Taifa la Uwezesheshaji wananchi Kiuchumi mlifuatilie kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI,” alisema Mhagama.

Katika hatua nyingine ameitaka mifuko/programu za uwezeshaji wanachi kiuchumi kutoa mikopo kwa riba nafuu tofauti na taasisi nyingine za kifedha, ambapo amebainisha kuwa takribani wajasiriamali 1,237,984 wamenufaika na mikopo ya mifuko hiyo na hadi kufikia Juni 2019 jumla shilingi bilioni 388.4 zimetolewa.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga ametoa wito kwa Taasisi za kifedha kuhakikisha zinajibu changamoto za wananchi huku akiwataka wananchi (wajasiriamali) walioshiriki maonesho haya kutumia vema fursa walizoziona katika mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili wakuze uchumi wao

Baadhi ya wanufaika wa mikopo wilaya ya Bariadi na Busega mkoani Simiyu na Chato Mkoani Geita  wamezishukuru Taasisi za kifedha zilizowakopesha mitaji jambo ambalo limewasaidia kuimarsisha shughui zao za kiuchumi wanazofanya ikiwa ni pamoja na kilimo na ufugaji.

“Naishukuru Benki ya AZANIA na wadhamini wangu Taasisi ya PASS kwa kuniwezesha kupata mkopo wa shilingi milioni 20, kuanzia sasa nitalima kisasa na nitaenda kuongeza miundombinu ya maji kwenye shamba langu maana nilikuwa nalima ekari 10 kwa kumwagilia badala ya ekari 30 nilizo nazo,” alisema Elisha Malugu kutoka wilayani Busega.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi(NEEC) Dkt. Festus Limbu amesema NEEC inaendelea kufuatilia agizo la Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alilolitoa Juni 2019 la kila mkoa kuwa na kituo cha uwezeshaji wananchi kiuchumi, lengo likiwa kuvifanya vituo hivyo kuwa kitovu cha uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Beng’ Issa amesema Maonesho haya yameshirikisha Taasisi 45, wajasiriamali zaidi ya 200 kutoka mikoa ya Simiyu, Mbeya, Pwani, Mwanza, Tabora, Kagera , Mara, Singida na Dar es Salaam na kutoka nchi jirani za Burundi na Kenya.

Maonesho ya tatu ya Mifuko/ Programu za Uwezeshaji na Vikundi vya Kifedha vya Kijamii chini ya Kauli Mbiu, “Mitaji ni Chachu ya Kujenga Uchumi wa Viwanda” yametanguliwa na maonesho ya kwanza yaliyofanyika Mbeya mwaka 2017, ambapo ya pili yalifanyika mwaka 2018  jijini Dodoma.


from MPEKUZI

Comments