Wastaafu Wakabidhi Mapendekezo Ya Kuboresha Zaidi Sekta Ya Mifugo Nchini

Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amepokea mapendekezo ya wataalamu wa mifugo wastaafu na wadau wa sekta ya binafsi yaliyotolewa ili kuboresha zaidi sekta ya mifugo nchini.

Akizungumza wakati akimkabidhi Katibu Mkuu Prof. Gabriel mapendekezo hayo katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar Es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati Teule ya wajumbe sita Dkt. Jonas Melewas, amemwambia katibu mkuu huyo kuwa mapendekezo yaliyotolewa ni Sita na kamati anayoingoza ambayo yanatokana na maazimio 14 yaliyotolewa kwenye kikao kilichofanyika Tarehe 7 Mwezi Oktoba 2019.

Dkt. Melewas ametaja mapendekezo hayo sita kuwa ni: Kusimamia tozo mbalimbali ikiwemo ya zao la ngozi na kuimarisha usimamizi wa Sheria na Kanuni kwa kuboresha mifumo ya ukaguzi ya uendeshaji, uzalishaji na biashara katika sekta ya mifugo.

Aidha Dkt. Melewas amefafanua pendekezo la tatu ni matumizi sahihi ya dawa za uogeshaji kudhibiti kupe na magonjwa yaambukizwayo na kupe kuzuia usugu na hasara kwa wafugaji.

Amebainisha mapendekezo mengine ni udhibiti wa magonjwa ya mifugo, kuongeza uzalishaji na tija katika ufugaji mbari za mifugo, mifumo ya ufugaji, uvunaji, biashara na masoko.

Akipokea mapendekezo hayo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara itatumia taratibu mbalimbali kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa na wastaafu hao na wadau wa sekta binafsi yanafanyiwa kazi na kwamba wizara pia inafanya kila jitihada kuhakikisha afya ya watanzania inaimarika kwa kutumia mazao ya mifugo ikiwemo nyama na maziwa kutoka kwenye mifugo isiyo na magonjwa.

Prof. Gabriel amefafanua kuwa Asilimia 60 ya magonjwa ya binadamu yanasababishwa na mifugo hivyo wizara itahakikisha inadhibiti magonjwa ya mifugo pamoja na kuhakikisha inasimamia vyema soko la mifugo nje ya nchi.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments