Rais Magufuli Ambana Mkurugenzi Nachingwea....Ataja Sababu za Kutumia magari ziara yake mkoani Lindi

Rais  Magufuli amewabana Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea (DC) Rukia Muwango na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bakari B Bakari baada ya wananchi kulalamikia ucheleweshwaji wa miradi ya maendeleo.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Oktoba 16, 2019 wakati Rais akihutubia wananchi katika wilaya ya Nachingwea ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa wa Lindi.

Baada ya hotuba za viongozi mbalimbali, Rais alimuomba Mwenyekiti wa CCM, Mzee Hashim Mkanjauka aeleze matatizo yote yanayowakabili wakazi wa Nachingwea.

Mkanjauka alianza kuelezea miradi ya maendeleo iliyokwama hali iliyowafanya wananchi waibuke kwa shangwe na hivyo kumfanya Rais atake kujua Zaidi kero hizo.

“Viongozi wetu siyo wakweli, miradi wilaya ya Nachingwea vijijini haitekelezeki, stendi ya wajasiriamali hakuna, soko halina kitu mkandarasi waliyempa hajamaliza, redio imenunuliwa na kufungwa kwa fedha za wananchi zaidi ya Sh100 milioni lakini haifanyi kazi. Maji yamekuja na mwenge yameondoka na mwenge Nachingwea ni wilaya kongwe,” amesema Mzee Mkanjauka.

Baada ya maelezo hayo Rais alimuita Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akimtaka atoe majibu ya kwanini miradi hiyo inasuasua na mingine imesimama kabisa.

“Sh200 milioni ilijenga sehemu ya kupumzikia wasafiri , mabanda 12 ya biashara sisi tulikuta imefungwa tuliwekeza kwa kuweka mabanda kwa mapato ya ndani ya Sh81 milioni, kujenga mabanda 26 kumalizia choo na kuanza kwa kuwa ni kubwa maeneo tuliyotenga kwa ajili ya wajasiriamali itabidi tuyapimie wameshapimiwa na wanaohitaji miundombinu ni mama lishe.”

Majibu hayo yalizalisha maswali zaidi kwamba ni kiasi gani hasa kilichotumika kwa upande wa soko pekee, Mkurugenzi huyo alijibu kuwa ni Sh71 milioni.

Baadaye Rais aliamua kushuka katika gari na kutembea mita kadhaa eneo la soko ili kujiridhisha kama kweli ujenzi unaendana na thamani ya fedha inayotajwa.

Baada ya kufika katika soko hilo na kuona hali halisi, alitaka kujua Sh71 milioni namna zilivyotumika lakini Mkurugenzi alionekana kujikanyaga namna alivyokuwa anajibu.

“Nawashukuru ndugu zangu wa Nachingwea kwa kuwa wakweli, ukweli humweka mtu huru, Tsh milioni 71 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa soko lakini mambo yanasuasua. Hayo mengine niachieni mimi nitafanya maamuzi.

“Tunahitaji watendaji wakali, huyu mkurugenzi wenu ameniuzi sana, anasema alikua anafanya kazi Marekani, sijui alikua anaokota makopo?

“Nafahamu shida mnayopitia barabara, ndiyo maana nimekuja na usafiri wa gari, ningeweza kuja na ‘helikopta’ lakini nimeamua kutumia barabara ili niyapate maumivu mnayoyapitia. Nataka niwahakikishie kuwa hii barabara ya kilometa 45 ya Nachingwea tutaijenga katika kiwango cha lami.

“Hii barabara tutaijenga kwa kiwango cha lami, kutoka Nachingwea – Ruangwa na Nanganga – Masasi, tumezoea kuona barabara za lami ni za mkoa kwa mkoa lakini sasa tunaanza kuunganisha hadi wilaya. Mliojenga pembezoni mwa barabara mjiandae kuhama bila fidia


from MPEKUZI

Comments