Atiwa Mbaroni kwa Tuhuma za Kumkatakata na Kumuua Mdogo wake

Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Mohamed Luambano (70) mkazi wa Mtelamwai wilayani Namtumbo kwa tuhuma za kumkata na kitu chenye ncha kali kichwani na kiganja cha mkono wa kulia mdogo wake, Abeid Luambano (65) na hatimaye kufariki dunia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alisema tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 2:00 usiku katika kitongoji cha Doroba kilichoko katika kijiji cha Mtelemwai.

Alisema inadaiwa siku ya tukio, Abeid alikutwa akiwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na pia kukatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiofahamika.

Maigwa alisema Abeid kabla ya kuuawa, alivamiwa ghafla na watu wasiojulikana nyumbani kwake na kisha kutolewa nje ya nyumba yake na kuanza kupigwa na kitu chenye ncha kali hadi kupoteza maisha.

Kutokana na tukio hilo, alisema Luambano ambaye ni kaka wa marehemu, amekamatwa kwa mahojiano zaidi kutokana na madai kwamba siku za karibuni kumekuwapo na kutoelewana kati ya ndugu hao.

Alisema ugomvu huo ulisababishwa na Abeid kuchomewa nyumba yake aliyokuwa akiishi akimtuhumu kaka yake na mtoto wake aliyetajwa kwa jina la Msajiri kuwa walikuwa wakimfanyia vitu vibaya.

Mtoto huyo wa Luambano amekimbia na kutokomea kusikojulikana baada ya tukio hilo la mauaji. Kamanda maigwa alisema juhudi za kumtafuta zinaendelea.


from MPEKUZI

Comments