Serikali Ya Kuboresha TBC Kufikia Viwango Vya Kimataifa

Anitha Jonas – WHUSM
Serikali imeahidi kuendelea kuboresha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa kuhakikisha linakuwa na muonekano bora kama mashirika ya Kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza wakati wa  Semina ya kuwajengea uwezo wabunge  kuhusu mpango wa serikali wa kuboresha mfumo wa Visimbusi kwa kutaka kuanzisha utaratibu wa kununua kifaa maalum kitakachobeba kifurushi ambacho kinaitwa ‘’CAM’ kifaa hicho kitatumika badala ya kununua zaidi ya kisimbusi kimoja.

Semina hiyo iliandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa wabunge wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

 ‘’Na serikali inampango endelevu wa kuboresha TBC na kuifanya ya kisasa zaidi na ndiyo maana tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikiongeza Bajeti ya Maendeleo kwa Shirika hilo na lengo ni kuifanya iwe yenye bora zaidi,’’alisema Shonza.

Akiendelea kuzungumza katika Semina hiyo Mheshimiwa Shonza alitoa wito kwa wanasiasa wote wa vyama vya upinzani  kujitokeza na kukitumia chombo cha TBC kwani shirika hilo ni la umma na halina ubaguzi kwa wanachama wa upinzani kama inavyosemekana kwani linaendeshwa kwa kodi za wananchi.

Kwa upande Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maeneleo ya Jamii Mhe.Peter Serukamba  alitoa rai kwa uongozi wa TBC kuhakikisha unatumia wapiga picha wenye weledi wakati wa uandaaji wa Makala za utalii kwa ajili ya Chaneli ya Utalii ya TANZANIA SAFARI CHANELI  kama chaneli nyingine za wadau wa utalii.

Halikadhalika nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe.Juma Nkamia alitoa angalizo kwa uongozi wa TCRA kufuatilia kwa umakini Maudhui ya Redio za Kijamii kwani redio hizo zisipofuatiliwa kwa karibu zinaweza kuleta changamoto hivyo ni vyema waweke mkakati madhubuti wa kufuatilia vituo hivyo.


from MPEKUZI

Comments