Reli Ya SGR Kuinua Pato La Taifa Kupitia Sekta Ya Mifugo Nchini

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ufufuaji wa reli ya zamani ni mkombozi mkubwa kwa wafugaji na wafanyabiara ya mifugo katika kupunguza gharama ya kufikia masoko na namna ya kufikia masoko hayo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, wakati alipotembelea ujenzi wa reli ya SGR pamoja na eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya bandari kavu ambapo pia kuna eneo maalum lilmetengwa kwa ajili ya kushushia na kupakia mifugo katika shamba la kupumzishia mifugo la serikali lililopo katika Kata ya Kwala, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani Mhe. Ulega alisema ujenzi huo unapaswa kuendelea kuzingatia sekta ya mifugo kadri kazi inavyoendelea kufanyika.

“Reli ya zamani ilikuwa na miundombinu yote inayohusisha mifugo na reli yetu ya kisasa SGR iendelee kuhusisha mifugo na ufufuaji wa reli ya zamani uende sambamba na kujua kwamba malighafi yetu watanzania ni mifugo yetu.” Alisema Mhe. Ulega

Mhe. Ulega amesema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa mara utakapokamilika na kuanza kufanya kazi, pato la taifa litakuwa kupitia sekta ya mifugo kwa kuwa mifugo itakuwa inasafirishwa kwa haraka ambapo reli ya mizigo itakuwa na mwendokasi wa Kilometa 120 kwa saa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, aliyeambatana na Naibu Waziri Ulega amemuarifu kuwa wizara yake imepata mkopo wa bei nafuu wa Dola za Marekani Milioni 300 kwa ajili ya kufufua reli ya zamani hivyo wizara itahakikisha wakulima na wafugaji wanatumia ipasavyo reli ya kisasa (SGR) pamoja na reli ya zamani.

Mhe. Nditiye amemuomba Naibu Waziri Ulega kufikisha wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika eneo la bandari kavu lililopo Kata ya kwala wilayani Bagamoyo, ambalo limetengwa maaalum kwa ajili ya mifugo ili wataalam hao watoe muongozo wa michoro ya namna eneo hilo linavyopaswa kuwa ili kuwezesha mifugo hiyo kuwa katika mazingira inayostahili.

Aidha Mhe. Niditiye amemshukuru Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega kwa kuwa na mawazo mazuri ya namna reli hiyo ya kisasa inavyopaswa pia kuwa mkombozi kwa wafugaji kwa kuhakikisha miundombinu yote inayohusu mifugo katika usafirishaji inazingatiwa.

Naye Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania Bw. Maghembe Makoye ameishukuru serikali kwa ujenzi ya reli ya kisasa kwa kuwa mifugo itakuwa inasafirishwa kwa muda mfupi na kufika katika eneo husika ikiwa na afya njema.

Aidha Bw. Makoye amefafanua kuwa uwepo wa miundombinu ya kupakia na kushushia mifugo iendelee kuzingatiwa katika ujenzi huo kwa kuwa kwa wafugaji mifugo ni uchumi kwao na taifa kwa ujumla.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments