Mfuko wa Hati Fungani kutoa fursa kwa jamii kujikomboa kiuchumi

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya UTT AMIS inayomilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeanzisha huduma mpya ya Mfuko wa Hati Fungani ‘Bond Fund’ ili kuiwezesha jamii iweze kuzifikia fursa za uwekezaji na kujikomboa kiuchumi.
 
Kuanzishwa kwa mfuko huo kumeongeza idadi ya mifuko na kufikia sita yote ikisimamiwa na kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 2013 ikichukua jukumu ya usimamizi wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja kutoka kwa Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT).
 
Akiuzungumzia mfuko huo, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi Mbaga, alisema utatoa fursa kwa wawekezaji wadogo, wakati kuzifikia fursa za uwekezaji zilizokuwa zikifikiwa na wawekezaji wachache, wakubwa.
 
Alifafanua kuwa, baadhi ya bidhaa hizo zinaeleweka kirahisi ambapo namna ya kuzifikia, kuwekeza ni rahisi lakini wakati mwingine hazitoi faida shindani kwa wawekezaji. 
 
Alisema mfuko huo utaondoa changamoto ambazo huwakuta wawekezaji kwenye soko la fedha ambalo lina bidhaa nyingi zilizobuniwa ili kukidhi mahitaji tofauti ya watumiaji. 
 
“Mbali ya Mfuko wa Hati Fungani, UTT AMIS inasimamia mifuko mingine ya uwekezajiambayo ni Mfuko wa Umoja, Wekeza Maisha, Watoto, Kujikimu, Mfuko wa Ukwasi. 
 
“Kuanzishwa kwa Mfuko wa Hati Fungani kumetokana na mahitaji ya wawekezaji pamoja na uchambuzi wa bidhaa za kifedha zilizoko kwenye soko la mitaji kwa sasa,” alisema. 
 
Mbaga alisema mfuko huo utawekeza kwenye hati fungani zilizoorodheshwa katika soko la hisa kwa asilimia 90, asilimia 10 itakuwa kwenye uwekezaji wenye ukwasi mkubwa.
 
Lengo ni kuwawezesha wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha kutokana na uwekezaji wao waweze kufanya hivyo, kumfanya mwekezaji achague kama anapenda kukuza mtaji au kupokea gawio kila mwezi, kila miezi sita kulingana na hitaji lake.
 
Alisema kampuni hiyo pia inatoa huduma ya usimamizi wa mali za kifedha ili kukidhi mahitaji maalum kwa wawekezaji binafsi wa kipato cha kati, cha juu na taasisi. 
 
Aliongeza kuwa, baadhi ya wawekezaji hasa wadogo ni vigumu kuwekeza katika baadhi ya bidhaa kwenye soko la fedha, Mfuko wa Hati Fungani umeratibiwa ili kuondoa changamoto hizo. 
 
“Mwekezaji anapata faida sawa na wawekezaji wakubwa, akihitaji fedha anauza baadhi ya umiliki wake kwenye mfuko kwa utaratibu rahisi bila kupoteza faida aliyoipata.
 
“Mfuko pia unawafaa wawekezaji wakubwa kwani ina faida shindani, gharama ndogo za kuwekeza, ukwasi wa kutosha, usalama wa mtaji, hatari ndogo za uwekezaji,” alifafanua.
 
Alisema mfuko huo hutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza, kushiriki katika masoko ya mitaji, kufaidika na uwekezaji huo, umeanzishwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa kipato cha chini, kati na kipato cha juu. 
 
Mbaga alisema watu binafsi, kampuni, taasisi, vikundi rasmi wanaweza kushiriki katika uwekezaji kwenye mfuko huo, lengo ni kuwafanya wawekezaji wawe na ushiriki mpana kupitia uwekezaji wa vipande, kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba kupitia hati fungani na masoko ya fedha.
 
Mfuko huo unatoa fursa ya uwekezaji rahisi wa muda mrefu kwa wawekezaji wanaopenda kuwekeza ili kukuza mtaji, kupata gawio kila mwezi au baada ya miezi sita kama anavyohitaji. 
 
“Kimsingi Mfuko wa Hati Fungani una mipango miwili ya uwekezaji ili kukidhi matakwa tofauti ya wawekezaji, kuna mpango wa kukuza mtaji, gawio kila mwezi na gawio kila baada ya miezi sita.
 
“Mpango wa kukuza mtaji, gawio la mara kwa mara halitatolewa kwa wawekezaji badala yake faida iliyopatikana itarudishwa kwenye uwekezaji wa awali kwa kununua vipande vitakavyonunuliwa kwa bei ya wakati huo. 
 
“Mpango huo utawafaa wawekezaji wanaohitaji kuweka akiba kwa malengo maalum mfano kujenga nyumba au wafanyakazi wenye kipato na wangependa kuwa na fedha ya akiba kama dharura itatokea au kwa matumizi ya baadae wanaweza kuchagua mpango wa kukuza mtaji,” alisema.
 
Mbaga alifafanua kuwa, wawekezaji katika mpango huo wanaweza kuuza kiasi chochote cha uwekezaji kama watakidhi vigezo ya mfuko vinavyohusu uuzwaji wa vipande. 
Mpango wa gawio kila mwezi hutokana na mahitaji ya kifedha ya mwekezaji na anavyochagua kwenye fomu ya maombi ya kuwekeza kwenye mfuko. 
 
Wawekezaji ambao wanahitaji kuchukua faida kila mwezi mfano wastaafu wanaopata fedha zao za mkupuo, kuwekeza kwenye mfuko wanashauriwa kupokea gawio kila mwezi ili wapate kipato cha kuishi bila kupoteza fedha walizopata. 
 
Mbaga alisema wawekezaji wengine wanaopata fedha nyingi kwa mara moja mfano wachimba madini wadogo, wanaweza kuchagua kupata gawio kila mwezi ili waweze kuendesha shughuli zao bila kuathiri mtaji walioupata. 
 
Pia wawekezaji watakaojiunga na mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vyote ili mradi wawe wamekidhi vigezo vya mfuko vinavyohusu uuzwaji wa vipande vya mfuko. 
 
Wawekezaji wanaopata fedha nyingi kwa msimu kama wakulima wa mazao mbalimbali, wanaweza kuchagua gawio la kila miezi sita ili waweze kupata fedha wakati wa kuandaa mashamba yao, kulima na kuvuna ili waweze kuendesha shughuli zao, kufuata msimu bila kupoteza mtaji.
 
Akizungumzia gharama za kuwekeza, Mbaga alisema hakuna gharama yeyote wakati wa kujiunga au kujitoa kwenye Mfuko wa Hati Funganui, wawekezaji wataruhusiwa kununua, kuuza vipande kwa thamani halisi ya kipande itakayokuwepo. 
 
“Wawekezaji wote wa ndani na nje ya Tanzania kama Sheria ya Soko la Mitaji na Dhamana inavyoruhusu, wanaweza kuwekeza kwenye mfuko huu,” alifafanua.
 
Kuhusu ununuzi wa vipande, alisema vinaweza kununuliwa siku yoyote ya kazi isipokuwa kipindi cha kufunga vitabu ambacho hakitazidi siku saba za kazi.
 
Alisema kuanzia Septemba 16, mwaka huu hadi Oktoba 16, mwaka huu, itakuwa kipindi cha mauzo ya awali hivyo ni vizuri Watanzania wakachangamkia fursa hiyo.
 
Kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000 na thamani halisi ya kipande itakuwa sh. 100 ambapo maombi ya kununua vipande yanaweza kuwakilishwa katika tawi lolote la Benki ya CRDB; ofisi za madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam; Ofisi za Shirika la Posta au Wakala yoyote atakayeteuliwa na UTT AMIS.
 
“Uwekezaji katika mfuko huu kwa wawekezaji walio nje ya Tanzania, awasiliane na ofisi za madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam au ofisi za UTT AMIS ili kupata taarifa na muongozo zaidi.
 
Anaongeza kuwa, thamani ya mwanzo ya kipande itakuwa sh.  100. Thamani ya kuuza na kununua kipande itakuwa sawa na thamani halisi ya kipande bila gharama yoyote. 
 
Kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000 na hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu, hiyo ni fursa kwa kila Mtanzania ambapo baada ya muda wa mauzo ya awali, mwekezaji anaweza kuwekeza kuanzia sh. 5000, mara nyingi kadri awezavyo.
 
Malipo ya mauzo ya vipande yanaweza kufanywa kwa fedha taslimu au hundi ya benki itakayolipwa kwenye akaunti ya Mfuko wa Hati Fungani iliyopo Benki ya CRDB. 
 
“Wawekezaji wanaweza kwenda kwenye tawi lolote la Benki ya CRDB na kufanya malipo. Pia malipo yanaweza kufanyika kwa kupitia M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money,” alisema.
 
Mbaga alisema kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa Kukuza Mtaji ni vipande 500. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100, thamani ya chini ya vipande, mauzo itakuwa sh. 50,000.
 
Kuhusu mpango wa gawio kila mwezi, kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa mpango wa gawio kila mwezi ni vipande 100,000, thamani ya mwanzo ya kipande sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh. 10,000,000. 
 
Mpango wa gawio kila miezi sita, kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa gawio kila miezi sita ni vipande 50,000, thamani ya mwanzo kwa  kipande sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh. 5,000,000. 
 
Alitoa wito kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi akiwahimiza wawe sehemu ya uwekezaji katika mfuko huo mpya kwani una faida nyingi, hawapaswi kuwa na hofu.
MWISHO.



from MPEKUZI

Comments