Watumishi waamuriwa kujichangisha kununua mashine ya ultrasound iliyoibiwa Hospitalini

Kufuatia mashine ya Ultra sound kuibiwa katika Hospitali ya Wilaya Bariadi, Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga ameagiza wafanyakazi wote wa Hospitali hiyo kuchangishwa fedha kulingana na kiwango cha mshahara ili kununua mashine mpya yenye thamani ya Tsh. Million 30 .

Kiswaga ametoa siku saba kwa watumishi wote kuchanga kulingana na mishahara kwa kila mmoja kuhakikisha wananunua mashine hiyo.

Kikao hicho ambacho kilifanyika jana katika ukumbi wa hospitali hiyo, Kiswaga alimtaka Mganga Mkuu wa Halmashuari hiyo, Mkurugenzi wa Halmashuari kuhakikisha ikifika Agosti 21, wapeleke mashine hiyo Ofisini kwake.

“Kwa kuwa mashine hii iliibiwa mchana na ikaibiwa na vifaa vyake vyote, inaonyesha kuwa waliohusika ni wataalamu na kwa maana hiyo watumishi wote 137 wa hospitali hii mnahusika na wizi huu, hivyo nyie ni watuhimiwa wa kwanza wa wizi huu.

“Kila mmoja kuanzia kwa Mganga Mkuu wa Halmashuari mtachangia kulingana na kila mtu na mshahara wake, nataka ndani ya siku saba nikabidhiwe hiyo mashine, ambaye atagoma kuchangia huyo itakuwa halali yangu,” alisema Kiswaga.

Aidha alisema tabia ya wizi katika hospitali hiyo imekuwa sugu ambapo wahusika wakuu wamekuwa watumishi wake, hali ambayo alieleza hawezi kuivumilia kama kiongozi wa Wilaya.

“Siyo mara ya kwanza kutokea wizi kwenye hospitali hii, mlihusika na wizi wa darubini (Microscope) ambapo baadaye ilipatikana ikiwa juu ya mti imeninginizwa, mkaiba tena mashine ya kufulia nguo ambayo mpaka sasa haijapatikana na leo tena Ultrasound hii haiwezekani na wala haikubaliki,” aliongeza Kiswaga.

Alisema kitendo hicho ni uhujumu uchumi hivyo watumishi wote lazima wahusike katika kuhakikisha mashine hiyo inarudishwa kwa gharama zao.


from MPEKUZI

Comments