TAKUKURU Shinyanga yabaini kasoro mbalimbali katika usimamizi wa miradi ya Umma.

NA SALVATORY NTANDU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga imebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya Umma unaofanywa na baadhi ya Watumishi serikali katika miradi minne inayotekelezwa mkoani humo iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 600.

Hayo yamebainishwa jana na kaimu Mkuu wa (TAKUKURU) mkoa humo, Hussein Mussa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na utekelezaji wa majukumu wa taasisi hiyo kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2019.

Amesema baada ya kukagua miradi mbalimbali katika sekta za afya, elimu,  maji, miundombinu na nishati wamebaini ukiukwaji wa manunuzi unaofanywa na watumishi hao kwa lengo la kujinufaisha ambapo wanatumia fedha zilizopo katika (Force Account) kufanya manunuzi bila kufuata sheria.

Amefafanua kuwa  baada ya TAKUKURU kufuatilia manunuzi ya vifaa yanayofanywa kwa kutumia 'Force Account' imebaini kuwa kuna baadhi ya manunuzi yanayofanyika yana kasoro mbalimbali kinyume na kusudio la serikali .

Ameongeza kuwa  manunuzi mengi yamebainika kufanyika kwa bei ya juu kuliko bei iliyopo sokoni lakini pia baadhi ya watumishi wa umma wanaohusika kufanya manunuzi hujaza wao wenyewe hati msako hivyo kusababisha  kujaza hadi kampuni au jina la biashara hewa ili mradi kampuni au mfanyabiashara anayekusudia apate kazi.

Amesema Watumishi hao  wanafanya malipo makubwa ya matumizi ya vifaa tofauti na uhalisia wa vifaa wanavyopokea na kamati za ujenzi zilizoundwa kusimamia hazifanyi ushindani halisi wa bei za vifaa badala yake wanapanga bei kwa kumpa mfanyabiashara mmoja kujaza hati msako zote na kupanga bei bei wanayotaka hivyo kuiingizia serikali hasara

Husein ameitaja miradi iliyotembelewa na TAKUKURU kuwa ni elimu,afya,maji,miundombinu na nishati na kwamba mpaka sasa wameanzisha uchunguzi katika miradi minne yenye thamani ya shilingi 644,864,180 na ushahidi wa kutosha ukipatikana watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Hata hivyo ame zitaja idara zinazoongozwa kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa kuwa serikali za mitaa, polisi, mahakama, ushirika, elimu, sekta binafsi, maji, madini, misitu, mawasiliano, afya, ardhi na ujenzi.


from MPEKUZI

Comments