Mkutano Wa Mawaziri Wa Mambo Ya Nje Wa Nchi Wanachama Wa Jumuiya Ya Madola

Tanzania imeshiriki mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola ambao umelenga kujadili utekelezaji wa maazimio na vipaumbele vya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ikiwemo masuala ya utawala bora,usalama,biashara pamoja na namna kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira. 

Akichangia katika majadiliano juu ya taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyokubaliwa katika mkutano wa Marais na Wakuu wa Serikali wa Nchi wanachama wa umoja huo ulifanyika mwaka 2018 London,Uingereza, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amewaeleza Wajumbe wa Mkutano huo kuwa Tanzania imeendelea kutekeleza maazimio ya mkutano uliopita kwa kusimamia ipasavyo misingi ya demokrasia na utawala bora na haki za binadamu na pia imehakikisha kuwa inatoa huduma bora za kijamii kwa watu wote ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, na pia imeongeza bajeti ya na kusogeza karibu huduma za afya karibu na wananchi kwa kujenga hospitali na vituo vya afya, nyumba za watumishi wa afya na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Vile vile Mheshimiwa Kabudi aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama na pia kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini na mijini ili kuchochea maendeleo katika maeneo yote ya nchi.

Aidha ameongeza kuwa katika kutekeleza maazimio ya Umoja huo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na uchafuzi wa mazingira, Tanzania tayari imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia tarehe 1 Juni, 2019 na amewahakikishia wajumbe kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa chanya.

Awali wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi. Patricia Scotland amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo inafanya  mageuzi makubwa ya kiutawala ili iweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi miongoni mwa nchi wanachama.

Pia amesema kuwa Jumuiya ya Madola inaendelea kuunga mkono na kutekeleza kauli mbiu ya umoja wa mataifa ya “hakuna atakayeachwa nyuma” katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ili kuhakikisha nchi zote wanachama wa Jumuiya zinapiga hatua mbele za kimaendeleo hususani katika nyanja za kiuchumi,kisiasa na kijamii.

Bi. Scotland amewashukuru Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya hiyo kwa kuhudhuria kwa wingi katika mkutano huo na kuwataka kuendelea kushirikiana na sekretarieti ya jumuiya ili iweze kutekeleza malengo mahususi yanayoendana na mahitaji ya nchi wanachama.

Katika hatua nyingine, Wajumbe wa Mkutano huo wameridhishwa na taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Mhe. Richard Sezibera kuhusu maandalizi ya mkutano ujao wa Wakuu wa Serikali wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika Kigali nchini Rwanda mwaka 2020.


from MPEKUZI

Comments