Nape Ageuka Mbogo Kwa Waliohujumu Zao la Korosho

Mbunge wa Mtama,Nape Nnauye (CCM) ametaka wote waliohusika na kuhujumu Korosho wachukuliwe hatua na wasipochukuliwa ataleta kusudio jinsi walivyofanya mmoja mmoja.

Kauli hiyo ameitoa leo,Mei 20 bungeni,wakati akichangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, kwa mwaka wa fedha 2018-2019.

Nape amesema waliofanya mambo ya hovyo katika kuhujumu Korosho,Serikali inatakiwa iwachukulie hatua kali na isipofanya hivyo atakuja na kusudio jinsi walivyofanya mmoja mmoja

“Watu waliofanya hovyo wanajulikana na kama wasipochukua hatua wenyewe, wasipofanya tutaleta kusudio jinsi walivyofanya mmoja mmoja na jinsi ambavyo wanatakiwa kuchukua hatua kwa sababu waliyoyafanya ni kuhujumu,Korosho,wananchi lakini pia ni kuhujumu uchumi wa Nchi.

Nape amesema Rais alikuwa na nia njema lakini walioenda kuitekeleza wameenda kuiua sekta ya Korosho.

“Hivi tunavyoongea Mheshimiwa Spika bahati mbaya zoezi lilikuwa na dhulma,lilikuwa na rushwa lilikumbwa na ubabaishaji mwingi na uongo mwingi sana.

“Hivi tunavyoongea Jimbo la Mtama peke yake kwenye vyama vya msingi 11 wakulima ambao wana korosho chini ya tani 1500 ambao wamehakikiwa mashamba yao zaidi ya 1281 kwa miezi nane tangu Korosho yao ichukuliwe hawajapa hata senti tano.

“Lakini Korosho yao imechukuliwa hawana fedha za kutengeneza mashamba yao.

Nape alisema mapendekezo yake ni iletwe sheria ya Korosho yote ili ipitiwe upya.

“Kile kipengele tulichokinyofoa kimetuletea shida sana sasa leteni sheria yote tuipitie.

“Napendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aende kukagua atuletee ripoti hapa ndani namna zoezi lilovyoenda ili tuchukue hatua ya kuziba mapengo.

“Kama nilivyosema Rais wengi wamemdanganya sasa ni vizuri wawajibike na Mheshimiwa Spika ni vizuri tukawa ‘Specific’ si sahihi kuiingiza Serikali katika mambo yaliyofanyika hovyo.

“Leo tukiulizana Korosho yetu ipo wapi haiwezi kukaa zaidi ya miezi sita hapa nchini ikabaki salama mngetuambia kuna korosho sahihi, huu ni uongo na tukiendelea kuusema huu uongo na bado tunaendelea kubaki hatutabaki salama,amesema Nape.


from MPEKUZI

Comments