Jaji Mkuu Akishauri chama cha wanasheria cha Tanganyika Law Society (TLS) Kushirikiana Na Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amekishauri chama cha wanasheria cha Tanganyika Law Society (TLS) kushirikiana na Mahakama katika kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza na Rais wa TLS pamoja na ujumbe wake walipomtembelea jana ofisini kwake jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amesema Mahakama pamoja na chama hicho wanayo maeneo mengi ya kushirikiana pasipo kuingiliana katika majukumu yao.

Aidha, Jaji Mkuu pia amekishauri chama hicho kuwa na mpango kazi wa muda mrefu ili kuongeza ufanisi ndani ya chama hicho kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria, viongozi wa chama hicho hukaa madarakani kwa kipindi cha mwaka moja kabla ya uchaguzi kufanyika tena.

Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa katika utoaji wa haki, Jaji Mkuu amewataka Mawakili nao kupambana na rushwa kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.

“Zifanyieni kazi changamoto za rushwa na shirikianeni na Mahakama ya Tanzania kwa kuwa Mahakama ni mfumo wa kukosoana, alisema Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Rais wa TLS Mhe. Dkt. Rugemeleza Nshala ameiomba Mahakama ya Tanzania kushughulikia changamoto mbalimbali wanazokutana nazo Mawakili wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria Mahakamani ikiwemo kuchelewa kuanza kwa kesi mahakamani.

Rais huyo pia aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano inaoutoa kwa chama chake na kuahidi kufanya kazi zake kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.

Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezar Feleshi amewapongeza viongozi wapya wa TLS waliochaguliwa hivi karibuni na kuwashauri kufanya kazi kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.

“Mifumo yetu iko wazi nasi tuko tayari kufanya kazi nanyi kwa kuwa wote tunayo nia moja ya kumtumikia mwananchi”, alisema Jaji Kiongozi.

Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Hussein Kattanga amewashauri viongozi wa TLS kushirikiana na Mahakama katika kutatua changamoto mbalimbali za upatikanaji wa haki na kuwataka kuwasilisha hoja na malalamiko kwa kuwa Mahakama kwa sasa inapokea hoja, maoni na malalamiko ili kuboresha huduma zake.


from MPEKUZI

Comments