Waziri Mkuu Mgeni Rasmi Mechi Ya Taifa Stars Na The Uganda Cranes Jumapili Taifa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, atakuwa mgeni rasmi katika mechi ya kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Afrika kati ya wenyeji Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Uganda (Cranes) itakayochezwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars, Paul Makonda ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kuwa wanaamini ujio wa kiongozi huyo utaongeza morali kwa wachezaji kwa ajili ya kusaka ushindi katika mchezo huo.

Makonda alisema kuwa kamati yake inawaomba wazalendo kujitokeza kushangilia katika mechi hiyo, ambayo Tanzania inajiandaa kuweka historia nyingine ya kufuzu fainali hizo baada ya kukosa kwa miaka 39.

"Mgeni rasmi katika mechi hii kubwa na muhimu kwa nchi yetu atakuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, tunaamini kila kitu kitakwenda vema na ili tuweze kutimiza ndoto zetu, kila shabiki anatakiwa kufika uwanjani kuishangilia Taifa Stars," alisema Makonda.

Wakati huo huo, wasanii wa bongo flava, filamu, watangazaji na watu wengine mbalimbali maarufu akiwamo mrembo wa Tanzania wa mwaka 2006, Wema Sepetu walijitokeza jana kuhamasisha Watanzania kujitokeza kuishangilia Taifa Stars katika mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi.


from MPEKUZI

Comments