Waziri Lugola Ataka Biashara Haramu Ya Binadamu Idhibitiwe

Na Felix Mwagara, MOHA-Zanzibar.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameitaka Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu nchini, iongeze kasi ya kupambana na biashara hiyo ili iweze kudhibitiwa kwa kuwa inaichafua nchi.

Waziri Lugola, ambaye kesho anatarajia kufungua mkutano mkubwa wa mafunzo kwa watekelezaji wa sheria ya kuzuia biashara hiyo haramu, katika hoteli ya Ngalawa, mjini Unguja, Zanzibar, alisema wakati akijiandaa kufungua mafunzo hayo, lakini wahusika waweke mikakati thabiti ya kuidhibiti biashara hiyo.

Mafunzo hayo ambayo ni ya siku tano, yatatolewa kwa wadau wanaotekeleza sheria ya kuzuia na kupambana na Biashara hiyo, Maafisa Polisi, Uhamiaji, waendesha mashtaka, Mahakimu, Maafisa Ustawi Jamii na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s) yaliyopo Zanzibar.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Waziri Lugola alisema Mkutano huo ni muhimu kwa wadau hao kupata mafunzo ya kukabiliana na mapambano ya biashara hiyo haramu ambayo Wizara yake itaendelea kuidhibiti. 

“Nimealikwa kufungua mkutano huo, baada ya mafunzo hayo ya kitaalamu ambayo nimeambiwa yatakuwa ya siku tano, naamini maafisa watakaopewa mafunzo hayo kutoka Wizara yangu na maafisa wengine wa Serikali kutoka sehemu mbalimbali nchini, pamoja na NGO’s za hapa Zanzibar watakuwa wamepikwa na kuiva na hatimaye watatusaidia katika kutekeleza sheria ya kuzuia biashara hii haramu ya usafirishaji wa binadamu,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara hiyo Haramu kutoka Wizara hiyo, Separatus Fella, alisema zaidi ya washiriki 80 watapewa mafunzo hayo na anamatarajio makubwa elimu watakayopewa itazaa matunda.

Fella alisema washiriki watapewa mafunzo mbalimbali katika semina hiyo itakayofanyika Kesho Machi 25, 2019, ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa zikiwemo, washiriki kujua kutofautisha makosa ya biashara haramu ya usafirishaji binadamu na mengine, na namna ya kupeleleza na kuendesha mashtaka.

“Pia washiriki watajifunza namna ya kuwalinda na kuwasaidia wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu, namna ya kuhoji watuhumiwa na mashahidi kwenye kesi za biashara haramu ya usafirishaji Binadamu,” alisema Fella.

Aidha, katika ufunguzi wa mafunzo hayo ambayo mgeni rasmi atakuwa Waziri Lugola, Fella alisema pia maafisa mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar watashiriki kwenye hafla ya ufunguzi huo.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo ni kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Marekani linalojihusisha na Masuala ya Utafiti (RTI).


from MPEKUZI

Comments