Rais Magufuli Aipongeza Taifa Stars Kwa Kufuzu Afcon

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufuzu kucheza fainali za michuano ya Afrika (AFCON 2019).

Mhe. Rais Magufuli ambaye alikuwa akifuatilia pambano hilo kupitia Luninga amerekodiwa picha ya video akifurahia ushindi baada ya pambano la Taifa Stars na Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) kumalizika kwa Taifa Stars kupata ushindi wa Magoli 3 kwa 0.

Mhe. Rais Magufuli amesema ushindi huo ni heshima kubwa kwa nchi na amewapongeza wachezaji na Watanzania wote kwa kufanikiwa kupeleka Timu yao ya Taifa katika fainali za AFCON ikiwa ni miaka 39 tangu ilipofanikiwa kufika hatua hiyo mwaka 1980.

Mchezo wa Taifa Stars na The Cranes umefanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Machi, 2019.


from MPEKUZI

Comments