Naibu waziri ulega asisitiza ukuaji wa sekta ya maziwa mkoani tanga

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefanya ziara ya siku moja Mkoani Tanga na kukutana na mkuu wa mkoa huo Bw. Martine Shigella pamoja na kuzungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU).

Mara baada ya kufika katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tanga, Mhe. Ulega alipokea taarifa ya mkoa iliyoainisha pia changamoto zilizopo katika sekta ya mifugo na uvuvi mkoani humo, ambapo Bw. Shigella ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzidi kutoa elimu kuhusu operesheni mbalimbali ambazo zinafanywa na wizara hiyo ili kuondoa usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza kwa wananchi hususan kwa wanaofanya shughuli za uvuvi katika mwambao wa Bahari ya Hindi.

“Niiombe Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwako mhe. naibu waziri kumekuwa na operesheni ambazo zinafanyika mara kwa mara na wakati mwingine watu kulalamika kuonewa, ni vyema operesheni hizi zikaenda sambamba na utoaji wa elimu ili kuondoa malalamiko ya wananchi.” Alisema Bw. Shigella

Aidha Bw. Shigella amemfahamisha Naibu Waziri Ulega ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ni fursa kubwa ya kuwezesha uzalishaji wa maziwa katika Mkoa wa Tanga kupitia matumizi ya bandari na ubia na kiwanda cha Tanga Fresh, hivyo wizara haina budi kuwawezesha wafugaji kupata ng’ombe wa kisasa ili kuzalisha maziwa kwa wingi na kufaidika na ushirikiano huo.

Akibainisha hatua mbalimbali za Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuboresha sekta ya maziwa kwa mkuu wa mkoa wa Tanga, Naibu Waziri Mhe. Abdallah Ulega amesema fursa mbalimbali zinazojitokeza mkoani Tanga ikiwemo ujumbe kutoka Rwanda kutumia bandari ya Tanga na kuweka ubia na kiwanda cha Tanga Fresh kutasaidia kukuza sekta ya maziwa mkoani humo.

“Kupitia uwekezaji huu uzalishaji wa maziwa utaongezeka na hivyo kuimarisha uchumi na kipato cha mwananchi kwa kuwa mahitaji ya maziwa yataongezeka hivyo lazima kuhamasisha zaidi ufugaji wa kisasa na wenye tija.” Alisema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amesema kuhusu operesheni mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kulalamikiwa na baadhi ya watu kuonewa, amesema masuala ya operesheni yanafanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba kuna baadhi ya mambo ambayo yanajitokeza katika operesheni hizo hivyo yanafanyiwa utafiti ili kuainisha yale ambayo yataonekana hayaendani na hali halisi ya wakati huu.

Katika hatua nyingine, mara baada ya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigella, Naibu Waziri Ulega alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh na baadae kuzungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU).

Akizungumza na wanachama hao Mhe. Ulega amebainisha kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Dawati la Sekta Binafsi imeiuanganisha Benki ya Kilimo (TADB) na TDCU kutoa mikopo ya ng’ombe takriban 300 kwa wafugaji wa Mkoa wa Tanga ili kukuza uzalishaji wa maziwa katika mkoa huo.

“Tuna nia ya kuwawezesha zaidi wafugaji na sisi kupitia Dawati la Sekta Binafsi lililoanzishwa mwezi Oktoba mwaka jana, tuliwapatia lengo la kuhahakisha tunazalisha kiwango cha upatikanaji wa maziwa katika taifa letu na kufanikisha mkopo kati ya TADB na TDCU ambapo sasa mnakwenda kupata ng’ombe bora kabisa takriban 300.”

Aidha Mhe. Ulega amewataka wafugaji kuhakikisha wanatunza mifugo yao vyema na kuwapatia chanjo ili waweze kupata maziwa bora ambayo ndiyo yatawezesha kiwanda cha Tanga Fresh kuzidi kukua na kutoa bidhaa bora zaidi zitokanazo na maziwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) Bw. Hamisi Mzee amemwambia Naibu Waziri Ulega kuwa chama kinahakikisha kiwanda cha Tanga Fresh kinazidi kuimarika kwa kufuata kanuni za ubora wa maziwa tangu yanapotoka kwa ng’ombe hadi kufika kiwandani hapo.

Amesema uwepo wa kiwanda hicho ni fursa pekee kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na maziwa hayo yamekuwa sehemu ya vitambulisho vikuu vya mkoa huo katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments