Mwenyekiti Halmashauri Ya Mji Njombe Aikingia Kifua Halmashauri Upotevu Wa Fedha Bilioni 5.5 Ya Ujenzi Wa Stendi

Na Amiri kilagalila
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe EDWIRN MWANZINGA  ameikingia kifua halmashauri kutokana na taarifa ya upotevu wa fedha shilingi bilioni 5.5 ya ujenzi wa stendi mpya ya halmashauri hiyo inayojengwa katika eneo la mji mwema mjini Njombe.

Akizungumza na mtandao huu meya huyo wa mji wa Njombe amesema kuwa anashangazwa na tuhuma hizo dhidi ya baadhi ya watumishi akiwemo afisa masuhuli kwa kuwa ameisoma taarifa ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali hivyo hakuna mahali ilipo onyesha  moja kwa moja kuna upotevu wa fedha hiyo.

“Ile ripoti kwa ujumla wake mimi nimeisoma na kuzipitia hoja zote na kimsingi katika hoja zile hakuna mahali walipoonyesha moja kwa moja kuna upotevu na hoja ya kwamba bilioni tano na point zimepotea kwa akili ya kawaida stendi isingekuwepo kwasababu stendi ile tunatumia karibu 5.7 bilioni kwa hiyo hizo zote zimepotea hapo sielewi na stendi ndio ile kama unavyoona tupo hatua ya mwisho kama ndio hivyo tumechukua za soko hamuoni soko linaedelea kwa hiyo hakuna ubadhilifu wowote ile ripoti imeonyesha mashaka tu, wananchi wawe na amani na tukiendelea kufanya hivi ni kuhatarisha mradi”alisema EDWIRN MWANZINGA

Mwanzinga ameongeza kuwa anakubaliana na hoja ya kucheleweshwa kwa mradi upande wa mkandarasi pamoja na halmashauri kwa kuwa mkurugenzi alikuwa akipokea maelekezo ya kuendelea na mkandarasi wa zamani aliyeshindwa kuendelea na mradi huo huku akipata maelekezo kutoka kwa viongozi wa ngazi ya mkoa,hivyo watumishi hao walikamatwa kwa kuonewa.

Mtandao huu umepata maoni kwa mmoja wa madiwani wa halmashauri hiyo ambaye ni diwani wa kata ya Ramadhani GEORGE SANGA,amesema kuwa tatizo kubwa kwa halmashauri hiyo mambo mengi yamekuwa yakiishia kwenye kamati ya fedha na wengine kushindwa kuonekana kama sehemu ya maamuzi.

“Ni wazi kwamba Njombe inahitaji kituo cha kisasa cha mabasi na ukizingatia ukweli kwamba mkoa unakua kwa kasi hasa mji wa Njombe, na ni wazi kwamba hakuna asiyejua ukamilikaji wake  umesua sua na kuacha maswali  kwa wananchi  lakini halmashauri imejitahidi kuhakikisha  unapatikana mbadala  wa kufanya ujenzi ili ukamilike kwa haraka  na kubadirisha mkandarasi ilikuwa ni njia mojawapo japo kuwa sisi madiwani wakati mwingine tumekuwa  hatuonekani kama sehemu ya maamuzi huku mambo mengi yakiishia kwenye kamati ya fedha”alisema diwani SANGA

Aidha juzi Jumamosi mkuu wa mkoa wa Njombe CHRISTOPHER OLESENDEKA  aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote waliotajwa katika taarifa hiyo kwa kuisababishia serikali hasara  hiyo ya shilingi bilioni 5.5 bila kufuata taratibu ya sheria ya manunuzi na kuto kuachwa hata mmoja kuanzia afisa masuhuli wa mji wa Njombe.

“sasa naagiza vyombo vyangu vya ulinzi wachukue hatua za kisheria dhidi ya wote waliotajwa katika ripoti hii katika tuhuma zote zenye thamani ya shilingi bilioni tano na nusu kila mmoja aliyeisababishia serikali hasara na ambaye hakufuata taratibu ya sheria ya manunuzi asiachwe hata mmoja wote wachukuliwe hatua,watendaji wote wachunguzwe na uanze kwa afisa masuhuli mwenyewe na kwenda kwa wakuu wa idara waliotajwa mpaka kwenye kamati yenyewe ya fedha na utawala na hata walio hama wafuatwe huko huko waliko” alisema Olesendeka

Hata hivyo wakati Olesendeka akitoa maagizo hayo, Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe kwa kushirikiana na wakuu wa idara walishindwa kuhudhuria katika kikao cha dharula cha baraza maalumu la madiwani kilichoitishwa na mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher olesendeka kwa ajili ya kujadili hasara na upotevu wa fedha hiyo ya ujenzi wa kituo cha mabasi.

Akiwa ofisini kwake mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa aliomba kuitishwa  kwa mkutano wa baraza la madiwani ili kukutana na madiwani kuzungumzia taarifa ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida mkurugenzi wa halmashauri hiyo ILUMINATA MWENDA na wataalamu walitoroka kikao hicho ilihali taarifa hiyo wakiwa nayo zaidi ya mwezi mmoja bila kuchukuliwa hatua.

“Baada ya kupokea ripoti ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabau za serikali nilimuagiza katibu tawala kumuandikia barua mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya  mji,achukue hatua ya kuwasimamisha kazi  wafanyakazi 12 waliohusika na kutajwa katika ripoti ya mkaguzi na baada ya kumuandikia lakini pia katibu tawala alimuandikia barua aitishe mkutano wa baraza la madiwani lakini mkurugenzi mwenyewe ametoroka kikao changu na akawazuia wakuu wa idara wasiuhudhulie mkutano wangu ila nimefika pale mkurugenzi hayupo,wakuu wa idara hawapo na madiwani wakaondoka na kwa maana hiyo mkutano wangu ukawa haupo”alisema Olesendeka

OLESENDEKA alisema kuwa ripoti ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali imesema kuwa mwanzo ilipotangazwa Zabuni kwa mara ya kwanza ukiondoa majengo mawili yaani jengo la hotel na jengo la zimamoto ambayo kwa pamoja yalikuwa na gharama ya shilingi bilioni 1milioni 285 elfu 795 huku ukiondoa VAT mradi huo gharama za awali ulikuwa ni shilingi bilioni 6 milioni 366,889 elfu na 544 lakini gharama za mwisho za mradi huo ulikuja kujengwa katika awamu tatu.

Alisema awamu ya kwanza na ya pili ulitekelezwa na mkandarasi wa ujenzi kampuni ya MS masasi CONSTRUCTION na awamu ya pili ikipewa kampuni ya HEINEN INTERNATIONAL huku gharama za awamu ya kwanza,ya pili na ya tatu zikiwa ni shilingi bilioni 9 milioni 355 laki 6 na elfu 20 na 806 na hivyo kutengeneza ongezeko la shilingi bilioni 2 milioni 988 laki 7 na 31 elfu 269.

Aidha ripoti imeendelea kuainisha makosa yaliyofanywa na  kamati ya tathmini ya zabuni,halmashauri ya mji wa Njombe kwa kumbeba mmoja kati ya wakandarasi walioomba Zabuni na kumpa ushindi mtu ambaye hakustahili na kumuacha mtu aliyestahili na hivyo kusababisha hasara kwa halmashauri ya mji na serikali ya shilingi bilioni 1 milioni 114 na 427 elfu 853 kwa hiyo serikali imepata hasara ya mradi kujengwa kwa gharama ya takribani bilioni 2.9 na shilingi bilioni 1.1 kutokana na kamati ya tathmini ikishirikiana na PMU  kitengo cha manunuzi,ikishirikiana na kamati ya fedha na utawala kwa ridhaa ya afisa masuhuli ikaipa serikali hasara ya shilingi bilioni 1 milioni 114 laki 4 na 27 elfu 893.

Katika utekelezaji wa mradi huo awamu ya kwanza na ya pili kampuni ya MASASI CONSTRUCTION ililipwa shilingi milioni 101 laki 5 na 89 elfu 781 malipo ambayo kazi iliyofanyika haikuonekana.
Lakini pia shilingi milioni 390 laki 3 na 97 elfu na shilingi 41 ambazo zimelipwa kama fedha za dharula katika awamu ya kwanza na awamu ya pili ya ujenzi kwa kampuni ya  MASASI  wakati haikupaswa kuonekana shughuli ya dharula bali ilipaswa kuwa ni sehemu ya fedha ilipaswa kuingia kwenye mkataba.

Aliongeza kuwa kuna shilingi milioni 531 laki 3 na 44 elfu 148 ambazo zimelipwa  kwa kampuni ya MASASI bila kuwa na measurement shirt inayoweza kuainisha kazi iliyofanyika na inalingana na thamani ya fedha hizo pamoja na kwamba zipo kazi zilizofanyika.

Olesendeka alimaliza kuwa kwa pamoja hoja ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali zilitaka maelezo ya takribani shilingi bilioni 5 milioni 524 laki 9 na 68 elfu 347 sawa na bilioni 5.5 ya fedha za serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzani ambazo hazikuzingatia kanuni ya manunuzi zilizofanywa kwenye ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe, na hivyo mchakato mzima kuwa na harufu ya rushwa alimaliza Olesendeka.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Njombe SALUM HAMDUN akizungumza jana mjini hapa alikiri kushikiliwa kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe ILUMINATA MWENDA pamoja na wenzake sita bila kuwataja watuhumiwa wengine kwa sababu za kiupelelezi

“ni kweli  mkurugenzi yupo chini ya ulinzi wa jeshi la polisi tulimshikilia tangu jana (juzi) tunaendelea kumhoji na wenzake sita na tunaendelea kuwatafuta wengine kama namna mkuu wa mkoa alivyoagiza”alisema kamanda wa polisi

Kituo hicho cha mabasi kilianza kujengwa tangu mwaka 2013 lakini mpaka sasa hakijakamilika licha ya kuwa kwa sasa kipo katika hatua za mwisho kukamilika.


from MPEKUZI

Comments