Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali Ambaye Awali Alikuwa Upande wa Maalim Seif Atangaza Kumuunga Mkono Profesa Lipumba

Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali ambaye awali alikuwa akimuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad  ndani ya CUF, sasa ametangaza kumuunga mkono  mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Bobali ametangaza uamuzi wa kumuunga mkono Profesa Lipumba leo Jumanne Machi 19, 2019 wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za makao makuu ya Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Amesema wapo wengi watakaorudi kuungana na Profesa Lipumba na kusema hivi sasa ni wakati wa kukijenga chama hicho na walioondoka kwenda sehemu nyingine ni utashi wao.

"Nimerudi nyumbani baada ya msuguano uliodumu kwa miaka mitatu ndani ya CUF na uliokidhoofisha chama, nawaomba mnisamehe kwa yaliyotokea.

“Natoa rai kwa wabunge wenzangu, madiwani na wenyeviti tusikimbie chama chetu, natoa wito tuungane turudi nyumbani tuje tujenge chama chetu huko kwingine kunakoendewa hakuna mwelekeo wowote utakapopatikana,“

"Najua kuna wenzangu wanataka kurudi lakini wanashindwa wataanzia wapi, nawaambia mimi nimeonyesha njia waje wasiogope wakati ndio huu," amesema .

Kwa upande wake, Profesa Lipumba amesema hawana nia ya kuwafukuza uanachama wabunge hao bali wanataka nidhamu ndani ya CUF .

Bobali amechukua uamuzi huo wakati leo Jumanne Maalim Seif pamoja na viongozi mbalimbali waliokuwa CUF wamekabidhiwa kadi za uanachama wa ACT- Wazalendo.


from MPEKUZI

Comments