Koffi Olomide ahukumiwa miaka miwili jela kwa kosa la unyanyasaji wanawake kingono

Msanii wa muziki mkongwe nchini DR Congo, Koffi Olomidé, amehukumiwa miaka miwili jela au kulipa faini ya Euro 5,000 baada ya kukutwa na hatia ya unyanyasaji kingono, moja ya waliokuwa Dancers wake miaka 15 iliyopita.

Hukumu hiyo imetolewa jana na mahakama ya Nanterre mjini Paris, Ufaransa.

Hata hivyo, wakati wa hukumu hiyo inasomwa, Koffi Olomide hakuwepo mahakamani hapo.

Olomidé, mwenye umri wa miaka 62, ametakiwa alipe Euro 5,000 kwa madhara aliyomsababishia mwanamke huyo.

Wakili wa Olomidé amepongeza uamuzi huo na kuutaja kuwa ushindi, akiwaarifu waandishi wa  habari kwamba uamuzi huo utachangia kuondolewa waranti ya kimataifa ya kumkamata.

Koffi Olomidé ni nyota wa muziki wa mtindo wa rumba na soukous ambao ni maarufu sana barani Afrika.

Mwaka 2012, Olomidé alishtakiwa kwa mara ya kwanza kwa makosa ya ubakaji na unyanyasaji kingono, lakini alikana makosa yote.

Awali, wanenguaji wanne aliokuwa akifanya nao kazi waliiambia mahakama kwamba mwanamuziki huyo, aliwanyanyasa kingono mara kadhaa kati ya mwaka 2002 na mwaka 2006. Walieleza kuwa unyanyasaji huo ulifanyika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Ufaransa.

Pia wanawake hao walieleza kwamba walizuiwa katika nyumba moja nje ya mji wa Paris na walifanikiwa kutoroka usiku wa Juni 2006, lakini hawakurudi DR Congo kutokana na kuogopa kutafutwa na kulipiziwa kisasi.


from MPEKUZI

Comments