Joshua Nassari Amfungulia Mashtaka Spika, Mahakama Yazuia Uchaguzi Kufanyika

Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari,  amefungua shauri la madai dhidi ya Spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma chini ya hati ya dharura kuomba kibali cha mahakama ili kufungua shauri la kufuta na kutengua uamuzi  wa Spika wa kumvua ubunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya bunge.

Akizungumza leo jijini Dodoma, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Dayness Lyimo, amesema kesi hiyo namba 22 ya mwaka 2019 inasikilizwa na Jaji Latifa Mansoor ambapo wajibu maombi ambao ni Spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamepewa siku saba kupeleka kiapo kinzani cha maombi hayo.

Nassari ambaye alikuwapo mahakamani hapo asubuhi anawakilishwa na mawakili watatu ambao ni Hekima Mwasipe, Jonathan Mndeme na Fred Kalonga. Upande wa walalamikiwa unawakilishwa na wakili wa Serikali, Masunga Kawahanda. Kesi hiyo itakwenda tena mahakamani Machi 27 kwa ajili ya kusikilizwa.

Aidha, mahakama hiyo imezuia kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo la Arumeru Mashariki hadi kesi ya maombi madogo ya kufungua kesi ya msingi ya kuomba kutengua uamuzi wa Spika wa kumfutia ubunge Joshua Nassari itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.



from MPEKUZI

Comments