Watu 34 washikiliwa na Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma mbalimbali

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu 34 kwa tuhuma mbalimbali katika misako iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mbeya kama ifuatavyo:-

KUINGIA NCHINI BILA KIBALI @ WAHAMIAJI HARAMU.
Mnamo tarehe 16.02.2019 majira ya saa 18:30 jioni huko eneo la mpakani, Kata ya Igawa, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. Polisi walifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu wawili raia wa nchini Ethiopia ambao ni DANIEL HARAM [29] na SADACK DADAGO [22] wakiwa wameingia nchini bila kibali. Taratibu za kisheria zinafanyika na upelelezi unaendelea.

KUPATIKANA NA POMBE MOSHI [GONGO]
Mnamo tarehe 17.02.2019 majira ya saa 11:30 asubuhi huko eneo na Kata ya Nkuyu, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa doria walimkamata JOHN MWASEBA [31] Mkazi wa Nkuyu Wilayani Kyela akiwa na Pombe Haramu ya Moshi @ Gongo ujazo wa lita 13. Uchunguzi unaonyesha kuwa mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa Pombe hiyo. Upelelezi unaendelea.

KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KIBALI.
Mnamo tarehe 16.02.2019 majira ya saa 21:00 usiku huko Mwakapangala, Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakifanya upekuzi katika magari mbalimbali walimkamata PRISCA PETER [32] mfanyabiashara, mkazi wa Uyole akiwa na:-
  1.     Pombe aina ya Prince chupa 20,
  2.     Kinywaji aina Power asili chupa 60,
  3.     Maziwa aina ya Super shake chupa 12,
  4.     Biscuits aina chiko dazan 2
Bidhaa hizo zote hazikulipiwa ushuru akiwa anazisafirisha kwa kutumia coaster ya abiria kutoka tunduma kuja Mbeya. Chanzo cha tukio hili ni kujipatia kipato kikubwa kwa kukwepa kulipa kodi ya mapato.

Mbinu iliyotumika ni kununua bidhaa hizo huko eneo la Black nchini Zambia katika duka la mtu mmoja raia wa Zambia [Jina linahifadhiwa] na kuvusha kwa njia za panya kwa kumtumia bodaboda ambaye husafirisha bidhaa hizo mpaka eneo la Sogea Stand alafu hupakia bidhaa hizo katika gari za abiria aina ya coaster na kuzipeleka wanakopanga kuzipeleka kwa wateja mbalimbali.

Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kufanya biashara hiyo. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika atafikishwa Mahakamani.

KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KIBALI.
Mnamo tarehe 16.02.2019 majira ya saa 13:00 mchana huko eneo la Kalumbulu, Kata ya Kyela, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa katika msako walimkamata STEWART NTULO akiwa amebeba:-
  1.     Mafuta aina ya Cook well lita 60 (sitini),
  2.     Kilo 60 (sitini) za sukari
Bidhaa hizo zilikamatwa zikiwa zinaingizwa nchini toka nchi jirani ya Malawi bila kuwa na kibali. Upelelezi unaendelea.

KUJERUHI.
Mnamo tarehe 15.02.2019 majira ya saa 21:00 usiku huko Galijembe, Kata ya Tembela, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya. MAJUTO MASHOWE [32] mkazi wa Ifiga alijeruhiwa kwa kukatwa kwa kitu butu kichwani na watu waliojichukulia sheria mkononi.

Chanzo cha tukio hilo ni kwamba mhanga ambaye anaishi Ifiga alienda kumchukua mtoto wake aitwaye BERNADETA MAJUTO [05] mwanafunzi wa Chekechea Shule ya Msingi Ngonde, mtoto ambaye huwa anampeleka shuleni hapo kila jumatatu na kwa sababu kuna umbali toka anakoishi hadi shuleni mtoto huyo huwa anabaki kwa mama yake mkubwa JOYCE BAHATI na huwa anamfuata kila ijumaa nakumleta jumatatu hivyo ijumaa alipoonekana akiwa amembeba mtoto huyo na raia wa pale standi bila kuuliza walihisi kuwa amemwiba mtoto huyo hivyo kumshambulia.

Mhanga amepatiwa PF3 na amelazwa wodi namba 2 katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na hali yake inaendelea kuimarika. Msako mkali wa kuwakamata watuhumiwa waliohusika na tukio hilo unaendelea na mara baada ya kuwakamata, watafikishwa katika vyombo vya sheria.

KUFANYA MKUSANYIKO USIO HALALI KWA NIA YA KUFANYA VITENDO VYA KISHIRIKINA.
Mnamo tarehe 16.02.2019 majira ya saa 17:40 jioni huko maeneo na Kata ya Itagano, Tarafa ya Sisimba ndani ya Jiji na Mkoa wa mbeya.  Askari Polisi waliwakamata watu kumi na nane [18] wakifanya mkusanyiko usio halali. Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na:-
  1.     JASSON SHONYELA [56]
  2.     NELSON MPESYA [48]
  3.     MICHAEL LABSON [32]
  4.     NELSON LEO [56]
  5.     JACKSON MWANDEMBA [60]
  6.      SIMON WALENJELA [65]
  7.      SAMSON MWANDEMBA [56]
  8.      MANFREDY MLAWIZI [60]
  9.      ARON MWANANYENE [48]
  10.      AMSHA NDELE [29]
  11.     ONESMO MAMBOLEO [45]
  12.     RASHID DAMSON [26]
  13.     TAZARA MWASHETWA [24]
  14.     MARIA SAMSON [60]
  15.     BALONGO WALENJELA [70]
  16.     SHIDA DAIMON [35]
  17.     FRANK JUMA [28]
  18.     DANIEL MWAMBIZA [78]
Wote wakazi wa Idimi Mkoani Mbeya. Watuhumiwa hao walikamatwa wakifanya mkusanyiko usio halali kwa nia ya kufanya vitendo vya kishirikina kwa kuwaleta waganga wa jadi (lambalamba) kwa kusadikiwa kuwa wanatoa uchawi kwa baadhi ya wananchi wa eneo hili wanaowatuhumu kuwa ni wachawi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria. Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa.  Upelelezi unaendelea.

KUPATIKANA NA MALI ZIDHANIWAZO KUWA ZA WIZI.
Mnamo tarehe 16.02.2019 majira ya saa 00:15 usiku huko mtaa wa Sae – Pipeline, Kata ya Ituha, Jiji na Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walimkamata JOSHUA FRANK MWAKILEMA [32] mkazi wa Sae Pipeline akiwa na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi ambazo ni:-
  1.     Printer mbili kubwa aina ya Epson,
  2.     Laptop mbili aina ya Accer na Fujistu,
  3.     UPS tano,
  4.     Polaroid Cd micro System moja,
  5.     Radio moja aina ya Polaroid,
  6.     Subwoofer mbili aina ya Sea Peano na Pioneer,
  7.     Radio aina ya Lasonic,
  8.     Feni moja aina ya Dolphin,
  9.     Dvd deck mbili pamoja,
  10.     Wino wa printer Pcs 29,
Mali zote hizo zinadhaniwa kuwa ni za wizi. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika, Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.


from MPEKUZI

Comments