Serikali Yalaani Mauaji na Matendo ya Kikatili kwa Watoto

Na WAMJW – DSM
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amelaani mauaji na matendo ya kikatili yote yanayofanywa dhidi ya Watoto, huku akivishukuru vyombo vya Dola kwa hatua za haraka wanazoendelea kuchukua katika kudhibiti matukio hayo.

Ameyasema hayo leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya Makazi ya Watoto wanaoishi katika Mazingira magumu yaliyopo Kurasini jijini Dar es salaam.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali haiwezi kuvumikia mambo yakikatili yanayofanywa dhidi ya Watoto na haki zao, hivyo itawachukulia hatua yeyote atakae bainika amekwenda kinyume na kuvunja sheria zinazomlinda mtoto.

“Tunalaani sana, mauaji haya ya Watoto, na tunavishukuru vyombo vya Dola vimeweza kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kwamba vinadhibiti matukio haya” alisema Dkt. Ndugulile

Mbali na hayo Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa Waganga wote wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kuacha kutumia viungo wala miili ya Watoto kama njia yakutatua matatizo kwa wateja wao, hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa watakao kaidi agizo hilo.

Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa Waganga wa Tiba Asili na Tiba mbadala wote ni lazima wahakikishe wanajisajili katika Mamlaka na Baraza husika ili kuepuka usumbufu na hatua kali dhidi yao pindi watakapobainika hawajafanya hivyo.

Ameongea kuwa Waganga wa Jadi watakaobainika  na kujihusisha na  shughuli zisizosajiliwa katika shughuli za Tiba Asili na Tiba Mbadala  watachukuliwa  hatua kali sana za kisheria dhidi yao na hata wale ambao watajihusisha pamoja na waganga hao. 

Dkt. Ndugulile pia ameutaka Uongozi wa Makazi ya watoto waishio katika mazingira magumu kuwajibika katika baadhi ya mambo ikiwemo masuala ya usafi wa mazingira , Mabweni na mavazi kwa watoto uzingatiwe na kuaagiza kuweka magodoro mapya, mashuka na chandarua  katika mabweni hayo.

Naye Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo Bi. Beatrice Mgumiro amesema kuwa makazi hayo yanajumla ya watoto 70 ambapo watoto 54 wapo katika makazi hayo na watoto 16 wapo wanasoma katika shule za bweni.

Bi. Beatrice amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa atatekeleza maagizo yote aliyompa na ameishukuru Serikali kwa uangalizi wa karibu wa watoto waishio katika mazingira magumu kwa kutoa huduma muhimu kwa watoto hao ikiwemo malazi chakula na elimu.


from MPEKUZI

Comments