Nape Afunguka Tena Sakata la Korosho

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesema kauli zinazotolewa na Serikali ndizo zinasababisha sintofahamu katika sakata zima la korosho.

Akizungumza katika kipindi cha Clouds 360 leo Jumatatu Februari 18,2019, Nape amesema kauli na matamko yanayotolewa na viongozi wa Serikali kuhusu suala hilo, yanachangia kuwavuruga wananchi na kusababisha malalamiko.

“Moja ya tatizo kubwa kwenye korosho ni kutokana na kauli zinazotolewa siku hadi siku, kauli ya Serikali inapaswa kuwa thabiti kuliko kutolewa matamko ambayo mwisho wa siku yanaweza kuwagawa wananchi.

“Serikali haichelewi wala haiwahi, sioni kama kuna haja ya kutoa kauli ambazo hazijafanyiwa utafiti wa kutosha, unasema kiasi fulani cha fedha kimenunua korosho wakati huku chini hazipo, inaweza ikatokea watu wa Mtama wakaona kumbe ni wao tu ndiyo hawajalipwa wengine wamelipwa,” amesema Nape.

Amesema, “Rais alikuwa na nia njema ila ninachokiona, vyombo vilivyo chini ya Rais havikujiandaa vizuri kutekeleza dhamira yake kuhusu korosho.”

Amesema kitendo cha kuondoa bodi ya korosho na kutoweka nyingine hadi sasa kilikuwa chanzo cha kutikisa mfumo.

Nape amesema, “mtikisiko huo haukuishia hapo bali kuliweka jeshi kusimamia kazi hiyo pamoja na fedha ya Serikali kutumika kuwalipa wakulima ni mambo yaliyochangia suala hilo kuwa zito.

“Hela inayotumika kulipa wakulima wa korosho ni ya Serikali na ina mlolongo mkubwa wa ‘vetting’ ndipo hapo linapokuja suala la uhakiki na kumbukumbu zangu zinanionyesha kila  palipo na uhakiki kuna ukakasi na ndiyo maana hata kwenye uhakiki wa korosho imeonekana kuna shida,” amesema


from MPEKUZI

Comments