Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Agoma Kukagua Ukarabati Wa Shule Ya Sekondari Pugu

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amelazimika kuahirisha kagua ukarabati wa Shule Kongwe ya Sekondari Pugu, Jijini Dar es Salaam baada ya uongozi wa mkoa na Manispaa ya Ilala kueleza kuwa hawajui lolote kuhusu ukarabati huo unao gharimu zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa madai kuwa hawajashirikishwa.

Dkt. Kijaji amechukua uamuzi huo baada ya Kaimu Katibu Tawala  wa Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Yokobeth Malisa, Afisa Mipango Manispaa ya Ilala Bw. Ando Mwankuga, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Dar es Salaam Mwl. George Lukoa  na Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Mwl. Jovinus Mutabuzi, wote kwa pamoja, kuukana mradi huo.

Mradi huo unatekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania-TEA chini ya ukandarasi wa Shirika la Nyumba Tanzania- NHC, lakini Mkataba wake pamoja na mawanda ya kazi inayotakiwa kufanyika haijulikani mkoani, Manispaa ya Ilala pamoja na uongozi wa shule.

"Mradi huu una changamoto kubwa, hatujawahi kuona mkataba wake kuanzia mkoani hadi Manispaa ya Ilala pamoja na uongozi wa shule, kwahiyo hatujui umegharimu kiasi gani na ni vitu gani viko kwenye Mkataba huo jambo linalotuwia vigumu kuuelezea" Alisema Bw. Ando Mwankuga

Bw. Mwankuga alieleza kuwa yeye ndiye mwenye taarifa ya miradi yote inayotekelezwa katika ngazi ya Manispaa ambayo kwa mujibu wa taratibu na kanuni hupitishwa kwenye vikao mbalimbali ikiwemo Kamati ya Ushauri ya Manispaa na Baraza la Madiwani, na kwamba mradi huo wa ukarabati wa shule ya Sekondari Pugu haujawahi kujadiliwa

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Jovenus Mutabuzi alieleza kuwa taarifa alizonazo ni za kuambiwa kwamba mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 900, lakini hajawahi kushirikishwa kikamilifu kuhusu ukarabati huo na yeye amekuwa akiwaona mafundi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa wakiingia kufanyakazi na kutoka shuleni hapo.

"Mhe. Naibu Waziri mimi naona tatizo kubwa hapa ni mawasiliano hafifu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Elimu Tanzania na Halmashauri Manispaa ya Ilala, ndio maana haya yote yamejitokeza" alisisitiza Mwl. Mutabuzi

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Yokobath Malisa, aliahidi kupeleka taarifa kwa Katibu Tawala wa mkoa huo ili aitishe vikao vya wadau wanaohusika ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Alieleza kuwa yeye binafsi akiwa miongozi mwa wasimamizi wa masuala ya miradi ya maendeleo ya mkoa wa Dar es Salaam hakuwa na taarifa ya uwepo wa mradi huo na haujawahi kuripotiwa mahali popote kwenye vikao.

Kwa upande wake Dkt. Kijaji ameelezea kushangazwa na hali hiyo kwamba mradi kama huo wenye thamani kubwa, utaratibu wake wa ushirikishanaji miongoni mwa wadau wanaohusika haujakaa vizuri jambo lililomfanya kuamua kusitisha zoezi la kukagua ukarabati wa shule hiyo.

"Kama hali ndiyo iko hivi! kila kiongozi hapa kuanzia mkoa, Manispaa hadi uongozi wa Shule mmeukana mradi huu kwamba hamuujui, wakati Mwalimu wa Takwimu wa Manispaa anasema anaufahamu pia juujuu, sasa mimi nitakagua nini? Tuondoke!" alielezea kwa masikitiko Dkt. Kijaji na kuahidi kulifanyiakazi suala hilo

Serikali imetoa zaidi ya  sh. bilioni 42 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Sekondari 42 kati ya shule 88 kongwe zilizopo nchini kote zikiwemo shule sita za Sekondari mkoani Dar es Salaam za Jangwani,  Azania, Tambaza, Zanaki, na Pugu.

Mwisho


from MPEKUZI

Comments