Makamu Wa Rais Aipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kusaidia Wakulima Wa Alizeti

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan  amepongeza juhudi za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kusaidia wakulima wadogo nchini hali inayoongeza uzalishaji na kuwaongezea kipato wakulima hao.

Makamu wa Rais aliyasema hayo wakati akikabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya Shilingi 1.285 Billioni zilizotolewa na TADB kwa ajili ya miradi ya kilimo cha Alizeti kwa wakulima 458 waliochini ya vyama vya ushirika (AMCOS) mkoani Singida.

Aliongeza kuwa wakulima waliopatiwa mkopo huo hawana budi kuutumia katika kuongeza tija ya uzalishaji ili kuweza kufikia malengo ya mkopo huo ambao umelenga kuchagiza kusaidia Sekta ya Mbegu za Mafuta nchini ili kutanzua changamoto za ukosefu wa mafuta hapa nchini.

Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa ushirika mkoani Singida kusimamia kwa makini mkopo huo ili utumike kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha unarudi kwa wakati ili uweze kusaidia wakulima wengine.

“Nawashi muwe waaminifu kwa kuutumia mkopo huu vizuri na kuurudisha kwa wakati ili kuwawezesha wakulima wengine nchini waweze kukopeshwa ili kuchagiza uzalishaji wa mazao ya kilimo,” aliongeza.

Mapema akizungumza na hadhara mjini Itigi ambapo mfano wa hundi hiyo ilipotolewa, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi alisema kuwa mkopo huo utachagiza hupatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda 144 ya kusindika mafuta ya alizeti vilivyopo mkoani humo.

“Kwa kipekee tunaishukuru TADB kwa kutoa mkopo kwa AMCOS hizi saba mkopo ambao umelenga kuongeza tija ya uzalishaji wa alizeti hali itakayochangia hupatikanaji wa malighafi ya uhakika ya viwanda vyetu,” alisema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara, Augustino Matutu Chacha, alisema kuwa kwa msimu huu wa mwaka 2018/2019, benki imeidhinisha mikopo ya jumla ya shilingi Bilioni 3.506 kwa miradi ya Kilimo ya Mkoa wa Singida pekee, ambapo Shilingi 1.285 Billioni zimetolewa kwa ajili ya miradi ya kilimo cha Alizeti kwa wakulima 458 waliochini ya vyama vya ushirika (AMCOS) na Shilingi 2.221 Billioni kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kusindika mbegu za mafuta ya alizeti kitakachojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

“Tunatambua Alizeti kama mojawapo ya mazao ya kimkakati kwa uchumi wa taifa letu na hasa kwa wananchi wa mikoa inayozalisha zao hili kwa wingi ikiwamo mkoa wa Singida. Zao hili la Alizeti lina fursa kubwa ya kuliingizia taifa fedha za kigeni na pia ni chanzo cha ajira kwa watu wapatao laki 3 na zaidi,” alisema.

Aliongeza kuwa Mkakati wa benki hiyo ni kuendelea kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa Alizeti zenye ubora kwa ajili ya kusaidia viwanda vya ndani kupata malighafi.

Aliongeza kuwa benki imefanya mazungumzo na inatarajia kukutana na wadau wasindikaji wa mafuta ya kula kwa lengo la kuandaa mpango shirikishi wa kutoa huduma za pembejeo na mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima.

“Benki ina mkakati wa kuwaunganisha wakulima na wasindikaji kwa ajili ya kupata huduma nafuu za pembejeo za kilimo,” aliongeza.

Mmoja wa wanufaika wa mkopo huo, amabaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika, Yahya Ramadhan alisema kuwa ujio wa Benki ya Kilimo umerudisha ari ya wakulima wa zao la alizeti mkoani Singida ambao kwa takribani miaka nane wameshindwa kulima kwa tija kutokana na ukosefu wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo za kilimo.

“Kwa hakika mkopo huu umerudisha ari ya wakulima kwani unatuhakikishia hupatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo kwa wakati hali itakayoongeza uzalishaji wa alizeti,” alisema.


from MPEKUZI

Comments