Maimu wa NIDA Augua....Ashindwa Kufika Mahakamani

Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho (Nida), Dickson Maimu, ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisabishia Serikali hasara ya Sh1.16 bilioni ni mgonjwa.

Mbali na Maimu mshtakiwa mwenzake mwingine katika kesi hiyo, Astery Ndege, ambaye ni  Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers,  pia ni mgonjwa.

Kutokana na kuugua  kwa washtakiwa hao ambao wote wako mahabusu, jana walishindwa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi yao, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.

Kesi hiyo ambayo inasikiizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Salum Ally jana Jumanne, Februari 19, 2019 ilitarajiwa washtakiwa  kusomewa maelezo ya mashahidi baada ya upelelezi kukamilikaa.

Hata hivyo mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai aliieleza mahakama kuwa kwa taarifa alizopewa na askari Magereza washtakiwa hao hawakuweza kufikishwa mahakamani kwa kuwa wanaumwa.

Kutokana na hali hiyo Swai aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia maendeleo ya afya ya wagonjwa hao.

Hakimu Ally amepanga kesi hiyo itajwe tena mahakamani hapo Machi 5 mwaka huu ili kuangalia maendeleo ya afya ya washtakiwa hao kabla ya kupangiwa tarehe nyingine ya kuendelea na hatua  ya  kesi hiyo kwa washtakiwa hao kusomewa maelezo ya mashahidi.

Mbali na Maimu na Ndege washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Avelin Momburi, aliyekuwa Meneja Biashara wa Nida; Mkurugenzi wa TEHEMA, Joseph Makani; Ofisa Usafirishaji,  George Ntalima; Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Wanakabiliwa na mashtaka 100 kati ya hayo, 24 yakiwa ni ya utakatishaji fedha zaidi ya Sh1.1 bilioni, 23ya kughushi nyaraka, 43 ya nyaraka za uwongo ili kumdanganya mwajiri wao, na mashataka matano ya kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh1.3 bilioni.

Mashtaka mengin ni ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu (mawili), shtaka moja la matumiz mabaya ya madaraka na mashtaka mawili ya kula njama.


from MPEKUZI

Comments