Lugola amuondoa Mkuu wa Kituo cha Polisi kwa kushindwa kusimamia misingi ya kazi

Na Felix Mwagara, MOHA-Karatu
WAZIRi wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemuagiza Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha kumuondoa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mang’ola wilayani Karatu kwa kushindwa kusimamia misingi ya kazi.

Lugola amesema amepokea malalamiko mengi kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Karatu.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Mji wa Karatu katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini humo, jana, Lugola amesema malalamiko yaliyotolewa na wananchi wilayani humo yanayonyesha Mkuu huyo wa Kituo ameshindwa kusimamia nidhamu.

“RPC nakuagiza umuondoe haraka iwezekanavyo Mkuu huyu wa Kituo hiki, mlete mwingine atakayejenga nidhamu upya ya askari katika kuwahudumia wananchi wa Mang’ola kwani kumekuwa na malalamiko mengi yanayotolewa na wananchi juu ya askari kushindwa kusimamia misingi ya kazi yao,” Alisema Lugola.

Pia Lugola amemwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, wafike katika Gereza la Mang’ola wilayani humo,  kuwaonyesha uongozi wa gereza hilo, eneo la kuchimba mtaro wa maji ili waachane na mtaro wanaoutumia wananchi ambao umekuwa ukileta mgogoro ndani ya eneo hilo.

Waziri Lugola, pia amemuagiza Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha kuwaondoa askari watatu waliolalamikiwa kuwazuia wananchi kutumia maji na kuwapiga wananchi.

Lugola alisema mgogoro huo umeketa matatizo, hivyo alimtaka Mkuu huyo wa Magereza kutuliza jali hiyo ili wananchi waweze kuyatumia maji hayo ambayo wanazuiwa na askari magereza.

“Nakuagiza kuzingatia yote niliyoyasema  katika kikao yaliyohusiana na kumaliza mgogoro huo baina ya askari na wananchi wanaodaiwa kupigwa na endapo watashindwa kutekeleza maagizo hayo nitaagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao,” alisema Lugola.

Wakizungumza katika mkutano huo wa hadhara, baadhi ya wananchi walitoa malalamiko jinsi askari magereza walivyowanyanyasa kwa kuwatisha kwa kutumia bunduki huku wakiwataja kwa majina yao kuwapiga raia na kuwanyang’anya upataji wa maji wakati wao sio wahusika wa zamu katika siku vitendo ambavyo vimefanya kuibua mgogoro mkubwa.

“Askari  wanakuja na bunduki wanakutishia mdomoni na kukusukuma wakidai hatutambuliki lakini tulipeleka malalamiko yetu ngazi husika ikiwemo kwa katibu tarafa ambaye alionya mara nyingi bila mafanikio,” alisema Jackson Qorou.

Katika ziara yake Mkoani Arusha, Lugola anakutana ma kero mbalimbali kupitia mikitano yake na wananchj hao na kuwataka askari wa vyombo vyake kuacha kulichafua Jeshi pamoja na Serikali kwa ujumla.


from MPEKUZI

Comments