Lipumba, Maalim Seif Waendelea Kunyukana....Pande Zote Mbili Zatangaza Kuteua Wajumbe Wapya wa Bodi

Chama Cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, umesema unatarajia kuitisha kikao cha kamati kuu ya chama hicho  waweze kuitisha kikao cha Baraza Kuu ambacho kitateua wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini.

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Saalam, kutengua uteuzi wa bodi ya wadhamini wa chama hicho kwa upande wa Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwa madai kuwa hawana sifa ya kuwa wajumbe wa bodi.

Wakati upande wa Profesa Lipumba ukisema hivyo, upande wa  Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad  nao umesema utateua wajumbe wengine ili kujaza nafasi hizo.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho, upande wa Lipumba, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema  wamekubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu na   wapo kwenye mchakato wa vikao vya juu vya taifa  waweze kufanya uamuzi ikiwamo kuteua wajumbe kama mahakama ilivyoagiza.

“Tupo kwenye mchakato wa kuitisha kikao cha Baraza Kuu ambako muda siyo mrefu tutateua majina ya bodi ya wadhamini na kuwapitisha.

“Kikao hicho pia kitashirikisha viongozi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama sheria inavyotutaka  tuweze kuwa na bodi bora itakayosimamia shughuli za chama,” alisema Kambaya.

Mkurugenzi huyo wa Habari   upande wa Lipumba, alisema   katika kipindi hiki ambacho wako kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho, watahakikisha wanapata bodi mpya mapema iwezekanavyo jambo ambalo linaweza kusaidia shughuli nyingine za chama kuendelea.

Alisema kwa mujibu wa uamuzi wa juzi, bodi zote mbili za Lipumba na Katibu Mkuu wa chama, Maalim Seif Sharif Hamad,  hazitambuliki katika sheria, hivyo basi kufanyika haraka kwa mchakato huo ni muhimu   chama kiweze kuwa na bodi ya wadhamini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama hicho,  Maalim Seif alisema uamuzi huo wa mahakama umewapa nguvu wanachama wao waliokuwa wakishuhudia mvutano uliozaa makundi ndani ya chama hicho.

“Tutafanya uteuzi mpya wa wajumbe wa bodi kwa kufuata vifungu vyote vya sheria na tutavipeleka Rita (Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi) ili isajiliwe. Ni matarajio yetu Rita itafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria

“Rita ni chombo muhimu katika nchi, tuna imani ya kuwa imejifunza mengi kutokana na hukumu ya jana (juzi) na italinda credibility (weledi),” alisema Maalim Seif.

Alisema uamuzi huo wa mahakama ni ushahidi tosha kuwa msajili wa Rita hakufanya kazi kwa ufanisi na kwamba hilo ni funzo kwa taasisi nyingine za Serikali katika kutekeleza majukumu yake bila kufuata msukumo.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa makini katika kufuata vipengele vyote vya kisheria katika utendaji kazi badala ya kufanya kwa mazoea huku akisisitiza kuwa uamuzi wa mahakama ulikuwa sahihi.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama, Maalim alisema ni wakati muafaka sasa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu fedha za ruzuku akidai kwamba masuala ya fedha yalifanywa na bodi hiyo kinyume na sheria.


from MPEKUZI

Comments