CHADEMA Wadai Kutotendewa Haki Mahakamani

Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limelaani nguvu kubwa inayotumiwa na Jeshi la Polisi mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi za viongozi wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Patrick ole Sosopi amesema Desemba 12, mwaka jana baraza hilo lilituma barua kwa Jaji Mkuu, juu ya matendo mbalimbali ambayo yanakiuka sheria za nchi, utawala wa sheria na kuingilia uhuru wa mahakama na haki za binadamu lakini amedai hawakujibiwa.

Aidha Sosopi ametumia fursa hiyo kumuomba Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kujibu barua hiyo.

"Desemba 12, 2018 tulimuandikia barua Jaji Mkuu kumwelezea ukiukwaji wa haki unaofanywa mahakamani lakini bado vitendo hivi vimeendelea kutia doa mhimili huo," ameeleza Sosopi.

"Mahakama ni mhimili unaojitegemea na sehemu huru kila mtu anapaswa kwenda kusikiliza kesi kama polisi wakiendelea kuingilia mhimili huu tutegemee mahakama zetu kugeuka mahakama za kijeshi," ameeleza.


Amesema Februari 18, 2019 wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na mweka hazina wa baraza la wanawake la chama hicho, Ester Matiko baadhi ya wanachama walikamatwa na wengine kupigwa walipojitokeza kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.


from MPEKUZI

Comments