Zao la Korosho Lapata Soko Nchini Algeria

Huenda kizungumkuti cha zao la Korosho nchini kikamalizwa kabisa, baada ya serikali kutangaza kupatikana kwa soko jipya la zao hilo nchini Algeria.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Damas Ndumbaro alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Algeria, Mhe. Saad Belabed, katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zilizopo jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Balozi Ndumbaro alieleza kuwa Algeria ipo tayari kununua korosho zote za Tanzania.

Dkt. Ndumbaro amesema mazungumzo hayo ni moja ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais  Dkt. John Joseph Magufuli za kuwakomboa kiuchumi Watanzania kwa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima nje ya nchi.

Serikali iliingilia kati taratibu za mauzo ya zao hilo kutokana na kuwa na mgogoro wa bei kati ya wakulima na wafanyabiashara, ambapo wafanyabiashara walitangaza kununua kwa sh 1,500 kwa kilo, bei ambayo ilipingwa vikali na wakulima.

Ndipo Rais Magufuli alipotangaza uamuzi wa serikali kununua korosho zote za wakulima kwa sh 3,300 kwa kilo na kuagiza korosho hizo zibanguliwe hapa nchini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.


from MPEKUZI

Comments