Rais Magufuli: Sitaacha kubadilisha Viongozi na hata Wewe Biteko ukifanya vibaya nitakutoa tu

Rais  Magufuli amesema hatochoka kufanya mabadiliko kwenye safu yake ya uongozi endapo ataona mambo hayaendi sawa kama anavyotaka.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 9, 2019 katika hafla fupi ya kuwaapisha viongozi aliowateua jana, akiwemo Waziri wa Madini, Dotto Biteko na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki.

Biteko amechukua nafasi ya Kairuki ambaye amedumu kwenye wizara hiyo kwa miezi 14 tangu ateuliwe Oktoba 2017.

Rais Magufuli amesema licha ya mabadiliko ambayo tayari ameyafanya kwenye Wizara ya Madini lakini sekta hiyo bado inaonekana kuwa na changamoto.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli changamoto hizo zinatokana na uongozi wa wizara hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo hali inayosababisha nchi kukosa fedha nyingi zinazotokana na madini.

“Sekta ya madini bado ina changamoto kubwa sana, ripoti inaonyesha nchi inayoongoza kwa kuuza dhahabu Afrika Mashariki si Tanzania wakati nchi yetu ndiyo inaongoza kuwa na dhahabu nyingi lazima tujiulize ni wapi tunakosea,” amesema Magufuli.

“Kuna udhaifu ambao Wizara ya Madini haiwezi kuukwepa. Kama tuna sheria nzuri, maeneo mengi ya kuchimba dhahabu,  je tumeshawahi kujiuliza wanapochimba wanauza wapi na wanapouza tunapata mapato asilimia ngapi?

“Kwenye  sheria kuna maelekezo ya kuanzishwa vituo vya madini je viko vingapi? Hivi vingesaidia kujua kiwango cha madini kinachopatikana na kinauzwa wapi?” Inauma unapoona kilo zaidi ya  300 zenye thamani ya zaidi ya bilioni 30 zinakamatwa zikisafirishwa. Wameshaiona Tanzania ni nchi ambayo unaweza kufanya lolote.” Amesema Rais Magufuli na kusisitriza;

“Nitaendelea kufanya mabadiliko kila mahali nitakapoona sijaridhishwa mhusika ataondoka, hata Biteko nimekuteua nikiona mambo hayaendi ninavyotaka utaondoka.”


from MPEKUZI

Comments